Jan 19, 2020 23:50 UTC
  • Jumatatu tarehe 20 Januari 2020

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na Januari 20 mwaka 2020.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita habari ya kukaribia safari ya kurejea nchini Imam Ruhullah Khomeini kutoka uhamishoni nje ya nchi ilienea kati ya wananchi wa Iran. Habari hiyo ilizusha furaha na vifijo kati ya matabaka mbalimbali ya wananchi. Mazungumzo na mijadala kuhusu suala la kurejea nchini Imam Khomeini na jinsi ya kumpokea shujaa huyo ilitanda kona zote na vikao vya wananchi.

Katika upande mwingine uamuzi wa Imam Khomeini wa kurejea nchini ulitikisa nguzo za utawala wa kifalme wa Shah. Vibaraka wa utawala huo walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa na wengi miongoni mwao walijiuzulu nyadhifa zao na kukimbilia nje ya nchi. Baadhi ya majenerali wa jeshi waliokuwa karibu na Shah waliwashambulia wananchi katika jitihada za mwisho za kulinda utawala huo wa kifalme. Mashambulizi hayo yalizidisha azma na moyo wa mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran.

Imam Khomeini

Tarehe 20 Januari miaka 100 iliyopita alizaliwa mtengeneza filamu mashuhuri wa Italia, Federico Fellini. Alikuwa mtayarishaji filamu mwenye mbinu makhsusi. Fellini alianza kuandika rasimu ya filamu (scenario) mwaka 1938 na baadaye akaingia katika uwanja wa kutayarisha filamu. Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia Fellini alishirikiana na mtengenezaji filamu mwingine wa Italia, Roberto Rossellini, katika utengenezaji wa filamu ya "Rome, Open City" (Roma, Mji Usiokuwa na Ulinzi). Miezi sita kabla ya kufariki dunia, Federico Fellini alitunukiwa tuzo ya fahari ya Oscar kutokana na kazi zake kubwa katika medani ya filamu. Filamu mashuhuri zaidi za Fellini ni "Saa Mbili Unusu", "Juliet of the Spirits" na "The Sweet Life".

Federico Fellini

Na siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kishia. Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini. Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari alielekea mjini Arak, Iran katika kipindi cha kuasisiwa chuo cha hauza cha mji huo na kujishughulisha na ukufunzi. Baadaye msomi huyo alishirikiana na Ayatullah Sheikh Abdul-Karim Hairi katika shughuli za tablighi na baada ya kuasisiwa hauza ya Qum, chini ya usimamizi wa Ayatullah Hairi Yazdi, Ayatullah Ahmad Khansari alikuwa imamu wa Swala ya jamaa katika chuo cha Faiziya mjini humo. Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea na kufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr. Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu.

Ayatullah Ahmad Khansari