Mar 01, 2020 02:36 UTC
  • Jumapili, tarehe Mosi Machi, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 6 Rajab, 1441 Hijiria, sawa na tarehe Mosi machi 2020.

Siku kama ya leo miaka 958 iliyopita Hassan as-Sabbah mmoja wa viongozi wakubwa wa Waislamu wa Shia Ismailiyah, alitwaa udhibiti wa ngome muhimu na imara ya Alamut, iliyo karibu na mji wa Qazvin, kaskazini mwa Iran. As-Sabbah ambaye kwa kipindi cha miaka 10 kabla ya hapo alikuwa akiwalingania watu kumfuata yeye, aliimarisha utawala wake baada ya kutwaa udhibiti wa ngome hiyo ambapo muda punde baadaye alipata kudhibiti miji mingine pia. Aidha baada ya kudhibiti ngome hiyo ya Alamut, kuliongezeka tabligh (linganio) za kuwataka watu wajiunge na madhehebu ya Shia Ismailiya na wafuasi wa wake walifanya mauaji dhidi ya viongozi wa utawala wa Seljuqi, akiwemo Khoja Nidham al-Mulk. Ngome ya Alamut iliendelea kuwa tegemeo la wafuasi wa Ismailiya nchini Iran hadi pale ilipoangukia mikononi mwa utawala wa Hulagu Khan mwaka 654 Hijiria. Hassan as-Sabbah alifariki dunia mwaka 518 Hijiria.

Hassan as-Sabbah

Siku kama ya leo miaka 925 iliyopita sawa na tarehe 6 Rajab mwaka 483 Hijiria, alifariki dunia Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri maarufu kwa jina la Ibn Hariri, mwanafasihi na mwandishi mashuhuri wa Kiirani aliyekuwa akiishi Basra nchini Iraq. Ibn Hariri ndiye mwandishi wa kitabu maarufu cha 'Maqamaat' ambacho ni cha aina yake katika taaluma ya fasihi ya Kiarabu. Katika kitabu hicho, Ibn Hariri alieleza siri za fasihi ya lugha ya Kiarabu katika kalibu ya hikaya na semi nyepesi za hekima.

Abu Muhammad Qasim bin Ali Basri

Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, ufalme wa siku mia moja wa Napoléon Bonaparte ulianza nchini Ufaransa baada ya Bonaparte kutoroka sehemu aliyokuwa amebaidishwa katika kisiwa cha Elba. Tarehe 27 mwezi Februari mwaka huohuo akiwa pamoja na wanajeshi elfu moja Napoleon Bonaparte alifanikiwa kutoroka katika kisiwa cha Elba ambako alikaa akiwa ubaidishoni kwa kipindi cha miezi kumi na kurejea Ufaransa na utawala wa kifalme ukaanza nchini humo.

Napoléon Bonaparte

Siku kama ya leo miaka 128 iliyopita yaani tarehe 1 Machi mwaka 1892 Miladia, alizaliwa mjini Tokyo mwandishi na mtaalamu mkubwa wa Japan anayejulikana kwa jina la "Rhunosuke Akutagawa". Mwandishi huyo anahesabika kuwa mmoja wa waasisi wa kanuni mpya za fasihi huko Japan. Akutagawa ameacha athari muhimu na miongoni mwake ni vitabu vya "Binti wa Buibui" na "Tushi Gun." Mwandishi huyo alifariki dunia mwaka 1927.

Rhunosuke Akutagawa

Siku kama ya leo miaka 122 iliyopita, kisiwa cha Puerto Rico kilichoko katika Bahari ya Atlantic kaskazini mwa Amerika ya Kusini, kilikaliwa kwa mabavu na vikosi vya majeshi ya Marekani baada ya kumalizika vita vya kikoloni vya Uhispania na Marekani. Baada ya Marekani kukitwaa kwa nguvu kisiwa hicho ilikifanya ghala kubwa la silaha, kiasi kwamba iliasisi kambi 13 za kijeshi kisiwani humo. Kisiwa hicho ambacho mara kwa mara hukumbwa na ukosefu wa amani, ni miongoni mwa maeneo yanayozungumza lugha ya Kihispania katika bara la America.

Kisiwa cha Puerto Rico