Mar 11, 2020 02:38 UTC
  • Jumatano, tarehe 11 Machi, 2020

Leo ni Jumatano tarehe 16 Rajab mwaka 1441 Hijria sawa na tarehe 11 Machi mwaka 2020.

Katika siku kama ya leo miaka 9 iliyopita yaani Machi 11 mwaka 2011, tetemeko la ardhi lililokuwa na ukubwa wa daraja 9 kwa kipimo cha rishta lililikumba eneo la Tohoku lililopo mkoa wa Miyagi Mashariki mwa Japan. Tetemeko hilo lilipelekea kuuawa watu elfu 12 na malaki ya wengine kubakia bila makazi kufuatia tetemeko hilo ambalo lilikuwa halijawahi kutokea mfano wake nchini humo kwa makumi ya miaka. Tetemeko hilo lilibomoa miundombinu, makazi ya raia na taasisi mbalimbali na kuiletea hasara ya mabilioni ya pesa nchi hiyo, kiasi kwamba kwa muda fulani, Japan ilikuwa katika hali mbaya ya kiuchumi. Tetemeko hilo lilizua mawimbi ya Tsunami yaliyokuwa na mwinuko wa mita 15, huku mawimbi mengine madogo madogo yakizikumba nchi nyingine za jirani kufuatia tetemeko hilo.

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa Yugoslavia ya zamani aliaga dunia akiwa korokoroni mjini Hague huko Uholanzi. Milosevic alitiwa mbaroni mwaka 2001 miezi tisa baada ya kuanguka utawala wake na kukabidhiwa kwa mahakama ya watenda jinai wa Yugoslavia ya zamani huko Hague. Slobodan Milosevic alijiunga na chama cha Kikomonisti cha Yugoslavia ya zamani akiwa kijana na kuwa Rais wa Jamhuri ya Serbia mwaka 1989. Dikteta huyo wa Yugoslavia ya zamani alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kushiriki katika mauaji ya umati dhidi ya maelfu ya Waislamu wa Bosnia.

Slobodan Milosevic

Miaka 16 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, miripuko ya mabomu matano ilitokea kwa wakati mmoja katika vituo kadhaa vya treni za chini ya ardhi au metro huko Madrid mji mkuu wa Uhispania na kuua karibu watu 200 na kujeruhi wengine 1000. Miripuko hiyo ilitambuliwa kuwa operesheni kubwa zaidi ya kigaidi kuwahi kutokea nchini Uhispania na Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Japokuwa serikali ya mrengo wa kulia ya Uhispania ililituhumu kundi linalotaka kujitenga eneo la Basque la ETA kuwa ndilo lililohusika na mashambulizi hayo ya kigaidi lakini kundi la al Qaida lilitoa taarifa likisema kuwa ndilo lililotekeleza hujuma hiyo.

Miaka 35 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, Mikhail Gorbachev ambaye wakati huo alikuwa mwanachama kijana zaidi katika Ofisi ya Kisiasa ya Chama cha Kikomunisti alitangazwa kuwa kiongozi wa chama hicho baada ya kufariki dunia Konstantin Chernenko. Kutangazwa kwa Gorbachev kuwa kiongozi wa chama hicho kulihitimisha mgogoro mkubwa katika ngazi za uongozi wa Urusi ya zamani ulioendelea kwa kipindi cha miaka mitatu. Hatua ya kuchaguliwa Gorbachev kuongoza chama hicho cha Kikomunisti ilikwenda sambamba na mabadiliko makubwa, ambayo hatimaye yalipelekea kusambaratika Umoja wa Kisovieti.

Mikhail Gorbachev

Siku kama ya leo miaka 1116 iliyopita kisiwa cha Malta maarufu kama "Herini ya Mediterania" kilitwaliwa na Waislamu na kuunganishwa na mamlaka ya nchi za Kiislamu. Utawala wa Waislamu wa kisiwa cha Malta uliendelea hadi mwaka 1091 yaani hadi zama za udhibiti wa kaumu ya Norman kisiwani humo. Malta ambayo inaundwa na visiwa vingi vidogo na vikubwa, ina ukubwa wa kilomita mraba 316 na jamii ya watu karibu nusu milioni. 

Kisiwa cha Malta