Mar 29, 2020 02:20 UTC
  • Jumapili, tarehe  29 Machi, 2020

Leo ni Jumapili tarehe 4 Sha'aban, 1441 Hijria, sawa na tarehe 29 Machi 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1415 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Hadhrat Abbas Bin Ali Bin Abi Talib, mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul-Banina, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (as) baada ya kufariki dunia Bibi Fatima Zahra (as). Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama vile baba yake Imam Ali (as), kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa Mashahidi kiasi kwamba alisabilia katika ardhi ya Karbala kwa lengo la kumtetea yeye na risala yake kwa nguvu zake zote. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake katika elimu kuliwafanya watu wengi wamrejee kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Abul Fadhl Abbas inajulikana hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. Aidha katika siku ya kuzaliwa mtukufu huyo, watu wa Iran huwa wanawakumbuka na kuwaenzi mashujaa waliosimama imara katika vita vya kulazimishwa vya utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya Iran. Kwa mnasaba huu, Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa mkono wa baraka kwa Waislamu na wapigania uhuru kote duniani.

Mazazi ya Abul Fadhl Abbas

Siku kama ya leo miaka 1001 iliyopita, sawa na tarehe 4 Shaban 440 Hijiria, alifariki dunia Abu Said Abul-Khayr, mtaalamu wa elimu ya Kumjua Mwenyezi Mungu (irfan) na malenga wa Iran akiwa na umri wa miaka 83. Abu Said alizaliwa mwaka 357 Hijiria na kujifunza elimu ya hisabati na historia ya wafalme. Aidha alitabahari katika elimu za tafsiri ya Qur’ani, Hadithi na fiqhi (sheria za Kiislamu), huku akipata elimu ya irfani kutoka kwa wanazuoni mashuhuri wa elimu hiyo wa karne ya nne na ya tano Hijiria. Kitabu cha ‘Asraarut-Tawhid’ ni moja ya turathi za Abu Said Abul-Khayr. Aidha alipendelea sana kusoma mashairi.

bu Said Abul-Khayr

Siku kama ya leo miaka 447 iliyopita, yaani tarehe 29 Machi 1573 Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa alitoa amri ya kihistoria iliyojulikana kama amri ya uhuru, ambayo ilikuwa kwa maslahi ya Wakristo wa madhehebu ya Protestanti. Kwa mujibu wa amri hiyo, Waprotestanti wa Ufaransa ambao walijipatia ushindi kwenye vita vya nne dhidi ya Wakatoliki wa nchi hiyo, walikuwa huru kufanya sherehe, ibada na misa zao nchini humo. Vita vya nne vya kidini kati ya Wakatoliki na Waprotestanti vilianza tarehe 16 Julai mwaka 1572 na vilikuwa maarufu kwa jina la Vita vya La Rochelle.

Mfalme Charles wa Tisa wa Ufaransa

Siku kama ya leo miaka 344 iliyopita, vita kati ya Poland na Ufalme wa Othmania vilifikia tamati kwa ushindi wa ufalme huo sambamba na kutekwa sehemu ya ardhi ya Ukraine iliyokuwa chini ya utawala wa Poland. Vita hivyo vilianza mwaka 1671 kwa uchokozi wa Wapoland.

Siku kama ya leo miaka 248 iliyopita, alifariki dunia Emmanuel Swedenborg, aliyekuwa mwanafikra mkubwa na msomi wa Sweden. Swedenborg alizaliwa mwaka 1688 na baada ya kubobea kwenye taaluma ya hesabati, aliweza kuwa mhandisi mahiri nchini humo. Swedenborg hakutosheka na elimu hiyo bali aliongeza juhudi kubwa na kutokea kuwa mtaalamu pia kwenye elimu ya falsafa na irfani. Msingi wa falsafa ya msomi huyo ulikuwa kujitenga na dunia ya kimaada na kuingia zaidi katika ulimwengu wa kimaanawi. Kwa msingi huo Swedenborg aliamini kuwa kadiri mwanadamu anavyosafisha roho yake ndivyo anavyomuelewa na kumjua zaidi Mwenyezi Mungu. Mtaalamu huyo aliandika vitabu zaidi ya 50 kwa ajili ya kuweka wazi falsafa yake.

Emmanuel Swedenborg

Na siku kama hii ya leo miaka 118 iliyopita sawa na tarehe 29 Machi mwaka 1902 Miladia, alizaliwa mwandishi wa Kifaransa kwa jina la Marcel Ayme. Katika masomo yake ya awali Ayme alisomea uhandisi hata hivyo kutokana na kupatwa na maradhi aliachana na taaluma hiyo. Baadaye alijishughulisha na uandishi wa magazeti na taratibu akaanza kujihusisha na uandishi wa riwaya ambapo alitokea kuwa mashuhuri katika uwanja huo. Marcel Ayme ameandika vitabu kadhaa na miongoni mwavyo ni "Beautiful Image", na "The Green Mare".

Marcel Ayme