Alkhamisi, tarehe 9 Aprili, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 15 Shaabani 1441 Hijria sawa na Aprili 9 mwaka 2020.
Siku kama ya leo mika 1186 iliyopita alizaliwa Imam Mahdi (af) mwokozi wa ulimwengu katika mji wa Samarra kaskazini mwa Baghdad mji mkuu wa Iraq. Yeye ni mwana mpendwa wa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Miongoni mwa lakabu mashuhuri za Imam huyo wa Zama ni Mahdi, ambayo ina maana ya mtu aliyepewa hidaya na kuongozwa na Qaim, kwa maana ya msimamishaji mapambano. Imam Mahdi alipitisha miaka mitano ya kwanza ya uhai wake akiwa na baba yake mpendwa Imam Askari (as).
Alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu kama Imam baada ya kuuawa shahidi baba yake huyo mtukufu na kisha kughibu machoni pa walimwengu kutokana na amri ya Mwenyezi Mungu. Kwa muda wa miaka 69 mtukufu huyo alikuwa akiwasiliana na kuwaongoza Waislamu kupitia wawakilishi wake maalumu. Baada ya hapo na kwa amri ya Mwenyezi Mungu, Imam Mahdi alienda kwenye ghaiba kubwa na ya muda mrefu ambapo atadhihiri tena ulimwenguni wakati muwafaka ambao Mwenyezi Mungu ataona unafaa. Atakapodhihiri humu duniani, ataujaza ulimwengu kwa uadilifu na usawa baada ya kujaa dhuma na uonevu.

Siku kama ya leo miaka 1112 iliyopita, Ali bin Muhammad Samori mwakilishi wa nne wa Imam Mahdi (af), ambaye alikuwa mwanazuoni mcha-Mungu na mwenye fadhila nyingi aliaga dunia. Baada ya kwenda ghaiba, Imam kwa makumi ya miaka alikuwa akiwasiliana na watu kupitia wawakilishi maalumu. Katika mazungumzo yake ya mwisho na Imam wa Zama (af) Samori alipokea barua kutoka kwake ambayo ilikuwa ikisisitiza kwamba hangemteua mwakilishi mwingine baada yake. Baada ya kuaga dunia Samori, Imam aliwataka watu kuwafuata wanazuoni wajuzi wa masuala ya dini kuhusiana na mambo mapya ambayo yangejitokeza.

Siku kama ya leo miaka 394 iliyopita, alifariki dunia Francis Bacon, mwanafalsafa maarufu wa Uingereza akiwa na umri wa miaka 65. Bacon alizaliwa mjini London tarehe 22 Januari mwaka 1561 Miladia na akaanza kusoma elimu ya msingi akiwa kijana mdogo. Baba yake Francis Bacon alikuwa miongoni mwa watu wa karibu sana na mfalme wa wakati huo wa Uingereza. Ni kwa ajili hiyo ndio maana msomi huyo naye akafanya juhudi kubwa za kujikurubisha kwa mfalme ambapo hatimaye alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mjumbe wa baraza la kitaifa sambamba na kusimamia vyombo vya mahakama vya nchi hiyo. Hata hivyo haukupita muda ambapo bunge la Uingereza lilimtuhumu kufanya ubadhirifu mkubwa serikalini na hivyo kumnyang'anya mali zake zote. Aidha Bacon alihukumiwa kifungo cha maisha jela. Hata hivyo mfalme wa Uingereza alimsamehe huku akimalizia maisha yake yoye nje ya jiji la London. Ameandika vitabu vingi katika uga wa falsafa na mashairi.
Siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, vilimalizika vita vya ndani nchini Marekani maarufu kwa jina la 'Vita vya Kujitenga.' Vita hivyo vilianza tarehe 12 Aprili mwaka 1861 Miladia, baada ya kuingia madarakani Abraham Lincoln vikizihusisha pande mbili za majimbo ya kusini (ambayo yalikuwa ya mrengo wa kulia) na yale ya kaskazini (ambayo yalikuwa ya upinzani.) Vita hivyo vilivyodumu kwa miaka minne vilifikia tamati kwa ushindi wa upande wa kaskazini hapo tarehe tisa Aprili mwaka 1865, huku vikisababisha mauaji ya zaidi ya watu laki tano. Ni kwa kufikiwa ushindi huo, ndipo kukatangazwa rasmi marufuku ya utumwa nchini humo. Hata hivyo na licha ya kupita karne moja na nusu tangu kumalizika kwa wimbi hilo la utumwa, lakini bado kunaendelea kushuhudiwa ubaguzi wa rangi mkubwa hususan dhidi ya jamii ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.
Katika siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, utawala ghasibu wa Israel ulifanya mauaji ya kinyama katika kijiji cha Deir Yassin huko magharibi mwa Baitul Muqaddas. Mauaji hayo yalifanyika wakati wa vita vya kwanza vya Waarabu na Israel na yalitekelezwa na Wazayuni wa kundi la Irgun lililokuwa likiongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Israel Menachem Begin. Eneo la Deir Yassin lilikuwa na umuhimu mkubwa kwa Wazayuni kutokana na kuwa katika njia ya Baitul Muqaddas na karibu na pwani. Baada ya kukivamia kijiji cha Deir Yassin, Wazayuni hao waliwaua kinyama wakazi 270 ambao hawakuwa na hatia yoyote wa kijiji hicho. Mauaji hayo yaliwalazimisha Wapalestina wengi wa eneo hilo kukimbia makazi yao kwa kuhofia kukaririwa mauaji kama hayo ya kinyama.