Alkhamisi, tarehe 28 Mei, 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 5 Shawwal 1441 Hijiria, sawa na tarehe 28 Mei 2020 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita yaani sawa na tarehe 5 Shawwal mwaka 60 Hijria, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein (as) aliwasili katika mji wa Kufa moja ya miji ya Iraq, kwa shabaha ya kuwalingania wenyeji wa mji huo kwenye njia ya haki na kuchukua baia yao kwa ajili ya Imam Hussein (as). Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua nyingi Imam Hussein (as) wakimuomba aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein (as) iliyowakaribisha kujiunga na harakati ya kiongozi huyo. Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein lakini baadaye walikengeuka. Mwishowe watu hao walimuacha peke yake Muslim bin Aqil na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari wa utawala wa Bani Umayyah.
Muslim bin Aqil
Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1940 Miladia, Ubelgiji ambayo ilitangaza kutoegemea upande wowote mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ilitekwa na majeshi ya Kinazi ya Ujerumani. Majeshi ya Ubelgiji ambayo yalikuwa yakipata usaidizi wa Uingereza, yalisimamisha vita kutokana na amri ya Mfalme Leopold wa Tatu, licha ya kusimama kidete kwa muda wa siku 18 dhidi ya majeshi ya Kinazi ya Ujerumani. Hatua hiyo ya Mfalme Leopold, iliwakasirisha mno wananchi wa Ubelgiji na kuandaa mazingira ya kuondolewa kwake madarakani hapo mwaka 1951.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1964, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanzisha shughuli za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa manachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia. Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo hapo mwaka 1993.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi. Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa. Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.
Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1998, kwa mara ya kwanza Pakistan ilianza kufanya majaribio matano ya makombora ya nyuklia. Majaribio hayo yalifanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu, tokea hasimu wake yaani India ifanye majaribio yake ya kombora la nyuklia. Baada ya hapo nchi hizo mbili zimekuwa zikifanya kwa zamu majaribio yao ya makombora ya nyuklia. Amma cha kushangaza ni kuwa, majaribio ya nyuklia ya Pakistan yamekuwa yakizikasirisha mno nchi za Magharibi za Marekani na Ulaya, na kufikia hatua ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.