Jul 06, 2020 05:19 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii (1):  Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani

Karne ya 20 tunaweza kuipa jina la Karne ya Mapinduzi. Mapinduzi ya mwanzo makubwa yaliyotokea katika karne hiyo yalikuwa ya Urusi ya mwaka 1917, yakafuatiwa na mengine kama mapinduzi ya China, Cuba, Iran na Nicaragua. Lakini hakuna shaka kuwa, mapinduzi muhimu zaidi na ya kipekee zaidi katika karne ya 20 yalikuwa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliyotokea mwaka 1979.

Mbali na kuuporomosha muundo wa mfumo wa kifalme uliodumu kwa miaka 2500, mapinduzi hayo yalitoa changamoto kubwa kiuhakiki, kwa nadharia zilizozoeleka katika Sayansi za Jamii na Uhusiano wa Kimataifa. Mapinduzi ya Kiislamu, hayakuubadilisha kikamilifu muundo wa kisiasa, kijamii na kiuchumi tu wa utawala, lakini pia yalitoa mtikisiko kwa taaluma za kijamii na za uhusiano wa kimataifa. Si hayo tu, lakini mapinduzi hayo yalikuwa somo na funzo pia kwa harakati za kijamii katika nchi nyinginezo na kwa harakati za ukombozi za Waislamu na vilevile yalitoa mvuto kwa wananadharia wa Sayansi za Jamii na wa Uhusiano wa Kimataifa ulimwenguni.

Katika hotuba za Sala ya Ijumaa ya tarehe 9 Februari 1995 (20 Bahman 1374), Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria kuwa na hali ya kipekee Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kwa kusema: “Mapinduzi makubwa ya Kiislamu ya Iran, kwa hakika yalikuwa mapinduzi ya kipekee… kwa kweli mapinduzi haya, yalikuwa tofauti na mapinduzi mengine. Tofauti hii inaonekana katika namna ya kutokea kwake, na pia katika sababu iliyochochea harakati ya wananchi.”

Mpenzi msikilizaji, inakaribia miaka 40 sasa ya umri wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa inakaribia kwenye maadhimisho ya mwaka wa 40 wa kuasisiwa kwake. Mapinduzi ya Kiislamu ni mapinduzi maalumu na ya kipekee katika hali nyingi, huku taathira yake ikiendelea kuonekana. Kitu kimoja muhimu zaidi kinachoyapambanua Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengine makubwa duniani katika namna ya kutokea kwake, ni kuhusu kufutwa nafasi ya madola makubwa duniani ndani ya nchi hii. Madola hayo makubwa, ndiyo yaliyokuwa wapangaji na waongozaji wakuu wa sera na utawala nchini Iran katika kipindi chote cha miaka 150 ya karibuni. Madola makubwa ya dunia yalikuwa yakiigawanya Iran kupitia mikataba iliyofungwa baina yao.

 

Moja ya mikataba muhimu zaidi kati ya hiyo, ulikuwa wa mwaka 1907 uliosainiwa na Urusi na Uingereza, ambao uliigawanya Iran katika maeneo matatu. Mkataba wa mwaka 1919 uliosainiwa na Iran na Uingereza, ulioziweka taasisi zote za fedha na za kijeshi za Iran, pamoja na njia za reli na barabara kuu chini ya usimamizi wa Waingereza, ni mkataba mwingine ulioiweka Iran chini ya udhibiti wa dola la Magharibi. Pamoja na hayo, kilele cha uingiliaji wa madola ya Magharibi katika masuala ya ndani ya Iran kilikuwa ni mapinduzi ya kijeshi ya tarehe 19 Agosti 1953 (28 Mordad 1332) yaliyopangwa na kuongozwa kwa pamoja na Marekani na Uingereza na kuipindua serikali halali ya Waziri Mkuu Mohammad Mosaddeqh. Baada ya mapinduzi hayo, Marekani ikageuka kuwa mdau muhimu zaidi na mwenye taathira kubwa zaidi nchini Iran, kwa kila kitu kuwa chini ya usimamizi wake. Kupitia uungaji mkono wake wa kila hali kwa utawala wa Shah na kuulazimisha kupitisha sheria mbalimbali za kikoloni ikiwemo ya Capitulation (iliyomfanya Mmarekani yeyote yule awe na kinga ya kutoshtakiwa ndani ya Iran), serikali ya Marekani ilikuwa ndiyo mpangaji mkuu wa sera za Iran na ikawa inajidhaminia maslahi yake ya kifedha kupitia mapato ya mafuta ya Iran.

William Healy Sullivan, balozi wa mwisho wa Marekani nchini Iran ameandika yafuatayo katika kitabu kiitwacho “Kazi Maalum Nchini Iran“ kuhusu uwepo wa Marekani hapa nchini: “Kuhusu uhusiano wa Marekani na Iran, kuna mambo mawili yaliyoishughulisha zaidi akili yangu. Jambo la kwanza ni kuhusu namna shughuli zetu zilivyokuwa nchini Iran na mipango mikuu ya uuzaji vifaa na zana za kijeshi kwa Iran. Ujumbe wa washauri wetu wa kijeshi nchini Iran ulianza kazi zake katika hali ambayo, msingi wa sera kuu za Marekani zilizoainishwa mwanzoni mwa muongo wa 1970, ulikuwa ni kuizuia Iran silaha na zana za kijeshi bila ya mpaka wowote. Katika kipindi kile, ujumbe wetu wa kijeshi nchini Iran ndio uliokuwa pia ukishughulikia jukumu la ununuzi wa silaha kwa ajili ya nchi hiyo. Utaratibu uliotumika ni kuwa, maafisa wa Iran, kwa kushauriana na washauri wa Kimarekani, walikuwa wakiandaa orodha ya silaha zinazohitajiwa, kisha ujumbe wa kijeshi wa Marekani ukawa unanunua silaha hizo na kuikabidhi Iran. Ulipaji fedha za silaha hizo, halikuwa tatizo lolote, kwa pato la mafuta ya Iran lililokuwa likiongezeka kila leo.”

 

Ervand Abrahamian, mwanahistoria aliyeandika kitabu kiitwacho “Iran Baina ya Mapinduzi Mawili”, naye pia ameutaja uhusiano wa Marekani na Iran ya enzi za ufalme wa Kipahlavi kuwa ni “Uhusiano Maalum” na kuandika: "Mapinduzi ya 1789 ya Ufaransa na ya 1917 nchini Urusi yalitokea katika mazingira ambayo, mifumo ya tawala za nchi hizo mbili ilikuwa rahisi kudhurika, kwa sababu haikupata uungaji mkono wowote wa kigeni. Lakini utawala wa Shah wa Iran ulikuwa ukipata uungaji mkono wa kila hali wa madola ajinabi, hususan Marekani. Lakini pamoja na hayo Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yaliweza kupata ushindi mwezi Februari mwaka 1979." (Februari 1979) (Bahman 1357)

Katika mazingira hayo, pamoja na uungaji mkono wa madola makubwa kwa utawala wa kifalme nchini Iran, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran si tu yaliweza kutokea na kupata ushindi, lakini mapinduzi hayo yalisimama pia kukabiliana na kambi mbili kuu za Mashariki na Magharibi. Licha ya kambi hizo mbili za Mashariki na Magharibi, zilizokuwa zikiongozwa na Urusi na Marekani kuitawala dunia, na pamoja na kambi mbili hizo kuwa na sauti ya juu kisiasa, kiuchumi, kiidiolojia na hata kijeshi katika matukio yote ya kieneo na kimataifa, viongozi wa mapinduzi ya Iran walitamka kinagaubaga kuwa, kaulimbiu yao kuu katika sera za nje ni “Si Mashariki, Si Magharibi”; na kwa kujitangazia sera hiyo wakasimama kukabiliana na kambi mbili kuu zenye nguvu katika mfumo wa kimataifa. Kwa utaratibu huo, “Kujitawala na Kujitegemea” (Independence) ikawa moja ya kaulimbiu kuu za Mapinduzi ya Kiislamu; na kimsingi hasa ni kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa tukio lenye kujitegemea, kiasi cha kuvutia fikra za weledi, wasomi na wananadharia wote duniani. Na suala hilohilo la kujitawala na kujitegemea, ndiyo moja ya sababu kuu za kuendelezwa na kushadidishwa uadui na uhasama wa madola ya Magharibi na hasa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hata baada ya kupita miongo minne sasa. Kuweza kujitawala katika hali ambayo, Iran ni nchi yenye nafasi ya kipekee duniani, kwa kuwepo kwenye eneo la kijiografia lenye umuhimu wa kisiasa na kistratejia, ni moja ya nukta muhimu zaidi zinazoipambanua Iran ya kabla na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 (1357).../

 

Tags