Jul 14, 2020 10:13 UTC
  • Mapinduzi ya Kiislamu Katika Nadharia za Sayansi ya Jamii (4): Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojipambanua na mapinduzi mengine makubwa duniani

Mazungumzo yetu katika sehemu ya tatu ya kipindi hiki yaliishia pale tulipogusia mitazamo ya waandishi mbali mbali kuhusu nafasi ya dini katika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Tukasema, kwa mfano Jalal Derakhshe anaitakidi kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu, kinyume na mapinduzi mengine makubwa kama ya Ufaransa na Urusi, ambayo msingi wake ulikuwa ni kuitenganisha siasa na dini, yalijengeka kutokana na itikadi na imani za watu katika jamii juu ya dini; na Uislamu, ukiwa ni imani na itikadi ya moyoni waliyokuwa nayo wananchi wa Iran, ulikuwa na nafasi kuu katika kupatikana ushindi wa wananchi hao. Nikki Keddie, ni mwandishi mwingine aliyezungumzia nukta hiyo kwa kueleza kwamba, harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran, ilifanyika kwa lengo la kubadilisha vigezo vya kifikra na kiutamaduni vya Kimagharibi vilivyokuwa vimetawala katika anga ya jamii, na badala yake kuasisi mfumo unaoendana na chimbuko la utamaduni na ustaarabu wa jamii ya Waislamu wa Iran. Kwa kuzingatia kwamba utambulisho wa kihistoria na kiutamaduni wa taifa la Iran, kwa muda wa karne na karne ulikuwa umejengeka na kupata maana yake halisi kwa kufungamana na fikra na amali za kidini sambamba na kuhusishwa dini katika masuala yote ya maisha ya kijamii, uenezaji fikra yoyote iliyokuwa ikipuuza na kutoijali dini, ulisababisha migogoro na misuguano ya kifikra, ambayo taathira zake zilienea hadi kwenye nyuga zote za kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi za Iran.

Max Weber (kulia) na Emile Durkheim

Ifahamike pia kwamba, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, yalitokea katika muelekeo uliofuata mkondo tofauti kabisa na mtazamo uliokuwepo katika Sayansi ya Jamii ya Dini. Kwa kutoa mfano ni kuwa, nadharia ya kufuata kaida na mambo yaliyokubalika, kwa kimombo norms, ambayo wananafikra kama Max Weber na Emile Durkheim walikuwa wakiipigia upatu sana, ilipata changamoto kali ya kutiliwa shaka ukweli wake. Kwa mujibu wa nadharia ya wataalamu hao wa Sosiolojia, katika kufuata muelekeo wa mantiki yaani 'rationality', mambo yanayopewa utakatifu yaani 'sacred' katika jamii huwekwa kando, na nafasi yao kuchukuliwa na muelekeo huo wa mantiki. Hata hivyo kwa kujiri Mapinduzi ya Kiislamu, ukweli wa nadharia hiyo ulikabiliwa na changamoto kubwa, kwa sababu Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa ni harakati kuelekea kwenye kuyapa thamani na kuyaenzi matakatifu ya kidini. Mapinduzi ya Iran yalithibitisha kuwa jamii za watu si tu hazifuati mkondo wa kuelekea kwenye Usekulari, lakini hata nchi zilizokuwa kwenye hatua ya awali ya kufuata mambo yaliyokubalika na kuzoeleka, zimerejea kwenye hali ya kufuata mambo yenye utakatifu. Kutokana na hali hiyo, Mapinduzi ya Kiislamu yalibatilisha pia madai ya nadharia ya Umaksi. Kwa sababu Wamaksi walikuwa wakiitakidi kwamba, dini ni kasumba ya kuuelewesha umma wa watu na silaha iliyokuwa ikitumiwa na tabaka tawala kuhalilishia unyonyaji wake kwa tabaka la chini, na wala haina sifa za kuleta ukombozi kwa watu.

Kwa hivyo kipambanuzi muhimu zaidi na kilichoyapa hali ya kipekee zaidi Mapinduzi ya Iran ni harakati na muelekeo wake wa kuasisi jamii ya kidini; yaani katika hali ambapo mabadiliko yote makubwa ya kijamii ya zama za sasa, ama hayakujali hata kidogo nafasi ya kijamii ya dini au hata yalilenga kuidhoofisha na kuifuta dini katika mahusiano ya kiutu na kijamii, mapinduzi ya Iran yalifuata mkondo ulio kinyume kabisa na mielekeo ya kifikra ya ulimwengu wa Magharibi na kutoa taswira ya kipekee ya utambulisho wa kihistoria wa jamii ya Iran. Kwa hakika, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, mbali na kutilia mkazo mamlaka ya kujitawala ya wananchi, huku nukta hiyo ikiwa moja ya vielezo vyake vikuu, yanatilia mkazo pia nafasi na mamlaka ya utawala ya dini.

Maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nukta nyingine inayoyatafutisha Mapinduzi ya Kiislamu na mapinduzi mengine makubwa duniani ni hali ya kiuchumi na kijeshi uliyokuwa nayo utawala wa wakati huo. Mapinduzi ya Kiislamu yalitokea katika nchi ambayo, kutokana na uwezo wake wa kijeshi na kiuchuimi ilichaguliwa na Marekani, dola kuu la kambi ya Magharibi kuwa "Polisi wa Eneo." Kutokana na kupanda bei ya mafuta, utawala wa Kipahlavi ulikuwa na hali nzuri sana kifedha, na ukautumia utajiri huo kununulia silaha na zana za kisasa za kivita kutoka madola ya Magharibi. Uwezo na nguvu za kijeshi lilizokuwa nazo jeshi la utawala wa Shah ulipelekea jeshi hilo kujihusisha na operesheni hata za nje ya mipaka ya Iran, ikiwemo kuingilia kijeshi eneo la Dhafar la nchini Oman kwa ombi la mfalme wa nchi hiyo Sultan Qaboos bin Said ili kwenda kuzima uasi wa wapiganaji wa msituni wenye mielekeo ya mrengo wa kushoto waliokuwa wakipigania kujitenga. Utawala wa Kipahlavi ulikuwa na jeshi la askari 413,000 na kuwa moja ya nguvu kuu za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, lakini pamoja na kuwa katika mazingira hayo, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalitokea. Na hii ni pamoja na kwamba, katika mapinduzi ya Ufaransa na Urusi, wakati mapinduzi yalipokuwa yanakaribia kutokea, nchi hizo zilikuwa zinkaribia kufilisika kikamilifu kiuchumi; na kutokana na kushindwa mtawalia katika vita kadha wa kadha, kwa upande wa kijeshi pia zilikuwa dhaifu na katika hali ya kulega lega. Nchini Ufaransa, katika mwaka 1789, utawala wa nchi hiyo haukuwa na uwezo hata wa kudhamini mahitaji ya mkate kwa raia wake; na nchini Urusi pia, utawala wa Waromanov, ulikuwa umekwama kwenye kinamasi cha Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia, huku nao ukiyumba kwa kukosa uthabiti wa kisiasa, kijamii na kiuchumi.../

 

Tags