Alkhamisi tarehe 16 Julai mwaka 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 24 Mfunguo Pili Dhulqaada 1441 Hijria sawa na Julai 16 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1241 Imam Ridha (a.s) alianza safari yake kutoka Madina kuelekea Marv huko kaskazini mashariki mwa Iran ya zamani. Imam Ridha (a.s) alifanya safari hiyo kwa kulazimishwa na kushinikizwa na Maamun, khalifa na mtawala wa saba wa Bani Abbasi. Lengo la safari hiyo lilikuwa ni kumuweka Imam Ridha chini ya uangalizi. Maamun alitoa pendekezo kwa Imam huko Marv kwamba akubali kuwaa mrithi wake. Maamun alifanya hivyo ili kujionyesha kuwa ni mtu mwenye mapenzi na Watu wa Nyumba Tukufu ya Mtume Muhammad(s.a.w). Hata hivyo katika fursa mbalimbali Imam Ridha si tu kwamba alionyesha kuwa hakubali kushirikiana na utawala wa Bani Abbasi bali aliutambua utawala huo kuwa ni wa kupenda makuu na wa kidhalimu.

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita James Parkinson aligundua ugonjwa wa Parkinson na namna unavyotokea. Kwa sababu hiyo ugonjwa huo ulipewa jina la tabibu huyo. Dalili za ugonjwa huo ni kama vile kutetemeka sana na kwa muda mrefu kwa ulimi, kichwa na mikono na kushindwa kuvuta miguu wakati wa kutembea hususan katika kipindi cha uzeeni na pia kukakamaa misuli katika sehemu yoyote ya mwili. Ugonjwa wa Parkinson unasababishwa na baadhi ya matatizo katika ubongo na hadi kufikia sasa hakuna dawa mujarabu iliyopatikana kwa ajili ya kutibu maradhi hayo.

Miaka 75 iliyopita katika siku kama hii ya leo bomu la kwanza la nyuklia la Marekani liliripuliwa wakati wa majaribio. Marekani ilifanya jaribio hilo la bomu la nyuklia ili kujiandaa kuishambulia Japan kwa kutumia mabomu hayo. Wakati huo Japan ilikuwa ikipigana na madola makubwa na majeshi ya nchi waitifaki, ikiwemo Marekani.

Tarehe 26 Tir miaka 40 iliyopita Baraza la kwanza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza rasmi kazi zake. Kwa mujibu wa kifungu nambari 91 cha Katibu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa lengo la kulinda sheria za Kiislamu na kuhakikisha kwamba sheria zinazopasishwa na Bunge hazipingani na dini ya Uislamu na Katiba, kuliundwa baraza lililopewa jina la Baraza la Kulinda Katiba. Baraza hilo lina wanazuoni sita wa fiqhi na sheria za Kiislamu wanaoteuliwa na Kiongozi Mkuu wa Iran na wataalamu 6 wa sheria ambao huarifishwa bungeni na kupigiwa kura baada ya kuteuliwa na Idara ya Vyombo vya Mahakama. Wadhifa mkubwa zaidi wa baraza hilo ni kuhakikisha kwamba, sheria zinazopasishwa na Bunge hazipingani na sheria za Kiislamu na Katiba, kufasiri Katiba na kusimamia chaguzi mbalimbali hapa nchini.

Siku kama ya leo miaka 12 iliyopita harakati ya Hizbullah ya Lebanon kwa mara nyingine tena ilifanikiwa kupokea mateka watano na miili ya karibu mashahidi 200 wa Kilebanoni kutoka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel mkabala wa kukabidhi mabaki ya maiti za askari wawili wa Kizayuni. Ubadilishanaji huo wa miili na mateka hao ulifanyika kufuatia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya pande mbili hizo kwa usimamizi wa serikali ya Ujerumani. Nukta ya kushangaza katika oparesheni hiyo ni kwamba vyombo vya usalama na ujasusi vya utawala wa Kizayuni hadi dakika ya mwisho havikuwa na habari kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa mwanzoni mwa mapigano kati ya jeshi la utawala wa Kizayuni na wapiganaji wa Hizbullah. Shakhsia wengine kutoka makundi ya mapambano ya Lebanon pia walikuwa miongoni mwa mateka walioachiwa huru na utawala wa Kizayuni. Shakhsia muhimu zaidi kuliko wote alikuwa Samir Qantwari ambaye alipoteza karibu miaka 30 ya umri wake akiwa katika jela za utawala wa Kizayuni.
