Aug 06, 2020 04:30 UTC
  • Alkhamisi tarehe 6 Agosti mwaka 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Dhulhija mwaka 1441 Hijria sawa na Agosti 6 mwaka 2020.

Miaka 968 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abu Abdullah Muhammad bin Jiyan, mnajimu na mwanahisabati wa Kiislamu huko Andalusia. Alizaliwa mwaka 379 Hijiria huko Cordoba moja ya miji ya kale ya Uhispania na alisoma hadi kuhitimu katika mji huo huo. Baada ya hapo alikwenda katika mji mkuu wa Misri, Cairo na kuishi huko kwa miaka minne. Jiyani alikuwa na umahiri mkubwa katika elimu ya nujumi na miongoni mwa athari za mwanahisabati huyo ni kitabu chake cha nujumi ambacho kimetajwa katika makala ya 5 ya kitabu cha elementi cha baba wa jiometri, Euclid wa Ugiriki ya kale.

Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita, alizaliwa Alexander Fleming tabibu, mwanabiolojia na mtaalamu wa madawa wa Scotland. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, tabibu huyo pamoja na wasomi wenzake wawili Chain na Florey, waligundua dawa ya antibiotic ya Penicillin. Mwaka 1945, wasomi hao watatu kwa pamoja walitunukiwa tuzo ya Nobel katika elimu ya tiba kutokana na ugunduzi wao huo muhimu. Penicillin inatumika sana hivi sasa katika elimu ya tiba.

Alexander Fleming

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mara ya kwanza kabisa duniani Marekani iliushambulia vikali kwa mabomu ya nyuklia na kuusambaratisha mji wa Hiroshima huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya uharibifu iliyokuwa sawa na tani elfu 20 ya mada za milipuko za TNT. Katika mashambulizi hayo watu zaidi ya elfu 90 waliuawa na wengine 75 elfu kujeruhiwa. Athari mbaya za mabomu hayo ya nyuklia zingali zinashuhudiwa hadi hii leo huko Hiroshima licha ya kupita miaka mingi sasa tangu kufanyike mashambulizi hayo ya nyuklia ya Marekani. Muda mfupi baada ya kuushambulia mji wa Hiroshima, Marekani iliushambulia pia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Nagasaki huko huko Japan na kuilazimisha nchi hiyo kusalimu amri. Maafa hayo ya kutisha na kusikitisha yaliyofanywa na Marekani katika miji miwili ya Japan ambayo yanahesabiwa kuwa jinai kubwa zaidi ya kivita katika historia, yanaonyesha kuwa silaha za nyuklia ni wenzo hatari sana katika mikono ya nchi zinazopenda kujitanua duniani kama Marekani na ndiyo maana kuna udharura wa kusimamiwa na kudhibitiwa silaha hizo na taasisi husika, na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa ajili ya usalama wa dunia.

Hiroshima baada ya shambulizi la bomu la nyuklia la Marekani

Katika siku kama ya leo miaka 58 iliyopita Jamaica inayopatikana huko Amerika ya Kati ilipata uhuru. Jamaica iligunduliwa mwaka 1494 na mvumbuzi Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania kuanzia karne ya 16 hadi ya 18. Nchi hiyo baadaye ilikoloniwa na Uingereza; na maghasibu wa Ulaya wakawafukuza wenyeji wa kisiwa hicho na badala yake wakawachukua makumi ya maelfu ya watumwa weusi kwa ajili ya kuwalimia mashamba yao.

Jamaica

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Agosti 6, 1995, Profesa Kighoma Ali Malima aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha NRA katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania aliaga dunia. Malima alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani. Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 19 na mwanafunzi hodari alikatisha masomo yake ya sekondari ili ajiunge na TANU katika harakati za kuikomboa Tanganyika kutoka katika utumwa wa Waingereza. Hayati Profesa Malima, atakumbukwa na wapenda haki wengi nchini Tanzania kutokana na kupinga kwake dhulma. Profesa Kigoma Ali Malima aliaga dunia ghafla kwa njia ya kutatanisha huko mjini London Uingereza alikopitia kutoka Makka alikokwenda kufanya Umra, zikiwa zimepita siku chache tu tangu alipotangaza uamuzi wake wa kukihama chama tawala cha CCM kufuatia kujiuzulu wadhifa wa uwaziri katika serikali ya chama hicho. Suala hilo lilimfanya akasirikiwe sana na chama hicho cha CCM.