Dec 24, 2020 03:32 UTC
  • Alkhamisi, 24 Desemba, 2020

Leo ni Alkhamisi tarehe 9 Mfunguo Nane Jamadil-Awwal 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 24 Desemba 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 656 iliyopita yaani sawa na tarehe 9 Jamadil Awwal mwaka 786 Hijria, aliuawa shahidi faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza." Alizaliwa mwaka 734 Hijria katika mojawapo ya vijiji vya Jabal Amil huko nchini Lebanon. Alijifunza elimu mbalimbali kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake kama vile Allama Hilli. Mbali na elimu ya dini, Muhammad bin Jamaluddin pia alikuwa hodari katika taaluma za mashairi na fasihi. Katika miaka 52 ya umri wake uliojaa baraka, Shahidi wa Kwanza aliandika vitabu vingi, ikiwa ni pamoja na "Albaqiyatus-Swalihat" na "Allumuatu Dimashqiyya." Aliuawa na wapinzani wake wenye taasubi katika siku kama ya leo. ***

Muhammad bin Jamaluddin Makki Amili, mashuhuri kwa jina la "Shahidi wa Kwanza."

 

Katika siku kama ya leo miaka 496 iliyopita, aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460. Mwaka 1498, baharia huyo wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India. ***

Vasco da Gama

 

Siku kama ya leo miaka  171 iliyopita wanajeshi wa Ufaransa waliivamia ardhi ya Guinea huko magharibi mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa nchi hiyo tajiri kwa madini ya dhahabu kudhibitiwa na Ufaransa. Kampuni ya Dhahabu ya Pwani iliundwa huko Guinea kabla ya uvamizi huo ili kuandaa mazingira ya kuingia kimabavu Ufaransa nchini humo.***

Bendera ya Guinea

 

Miaka 155 iliyopita katika siku kama ya leo, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu zaidi, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, hususan raia weusi. Japokuwa kundi hilo la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limefanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi, kuzusha hofu na kutoa vitisho dhidi yao. Kundi hilo linaua hata wazungu wanaotetea haki za makundi mengine. Pamoja na hayo hakujafanyika juhudi kubwa nchini Marekani kwa ajili ya kung'oa kabisa mizizi ya kundi hilo la kibaguzi na lenye misimamo ya kuchupa mipaka. ***

Vasco da Gama

 

Na siku kama ya leo miaka 69 iliyopita nchi ya Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi akateuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikajipatia uhuru wake mwaka 1951. ***

Bendera ya Libya

 

Tags