Feb 03, 2022 03:13 UTC
  • Alkhamisi 3 Februari 2022

Leo ni Alkhamisi tarehe Mosi Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 3 Februari 2022.

Leo ni tarehe Mosi Rajab, mwezi uliojaa rehema na fadhila tele. Mwezi huu na miezi miwili inayofuata yaani Sha’aban na Ramadhan ni kipindi muhimu kwa ajili ya kujisafisha mwanadamu na kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kuhusiana na mwezi huu wa Rajab, Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mwezi wa Rajab ni mwezi mkubwa wa Mwenyezi Mungu…kupigana vita na makafiri ndani ya mwezi huu ni haramu. Rajab ni mwezi wa Mwenyezi Mungu, Sha’aban ni mwezi wangu na Ramadhan ni mwezi wa umma wangu.” Kufunga Saumu katika mwezi huu kumesisitizwa sana na kuna thawabu nyingi. Baadhi ya hadithi zimesisitiza sana kufunga Saumu na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu katika mwezi huu. Katika mwezi huu kuna matukio mawili muhimu. Tukio la kwanza ni kuzaliwa Imam Ali (as) tarehe 13 ya mwezi huu na tukio la pili ni kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad (saw) tarehe 27 ya mwezi huu wa Rajab.

Siku kama ya leo miaka 1386 iliyopita, kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia alizaliwa Imam Muhammad Baqir AS mjukuu mtukufu wa Mtume Muhammad (SAW) na mmoja wa Maimamu watoharibu kutoka katika kizazi chake. Imam Baqir AS alizaliwa katika mji mtakatifu wa Madina na kupata umashuhuri katika uwanja wa elimu, ambapo alikuwa akijibu maswali na masuala magumu ya zama na kwa sababu hiyo alipewa lakabu ya Baqir yaani mchimbua elimu. Kipindi cha Uimamu wa mtukufu huyo kiliambatana na kudhoofika kwa utawala wa Bani Umayyah suala ambalo lilimpa fursa nzuri ya kulea Waislamu wa zama hizo kifikra na kielimu. Imam Baqir (as) alisifika kwa ukarimu, kuwasamehe waliomkosea, kuwasaidia masikini na kuwatembelea wagonjwa.

Tarehe 3 Februari miaka 554 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa mashine ya uchapishaji, Johannes Gutenberg. Mvumbuzi huyo alizaliwa nchini Ujerumani lakini alihamia Strasbourg, Ufaransa na akaanza kujishughulisha na kazi za kiufundi. Mwaka 1443 au 1444 Gutenberg alifanikiwa kutengeneza mashine ya uchapishaji na kupiga hatua muhimu katika uchapishaji na uenezaji wa elimu na maarifa kati ya wanadamu. Katika zama zake, Johannes Gutenberg pia alichapisha kitabu cha Biblia maarufu kwa jina la' Gutenberg Bible.'

Johannes Gutenberg

Miaka 192 iliyopita katika siku kama ya leo, Ugiriki ilipata uhuru wake kutoka kwa utawala wa Othmania. Ugiriki ambayo kijiografia ipo kusini mashariki mwa Ulaya ni moja kati ya nchi zenye tamaduni kongwe duniani. Mwaka 338 kabla ya kuzaliwa Nabii Isa a.s, mfalme wa Macedonia aliivamia Ugiriki na karne moja baadaye nchi hiyo ikawa chini ya mamlaka ya utawala wa Roma na baadaye Roma ya Mashariki. Katika kipicdi chote cha karne ya 19, Ugiriki ilishuhudia mapigano vita na vurugu za ndani na nje. Hatimaye katika siku kama ya leo nchi hiyo ikajipatia uhuru.

Bendera ya Ugiriki

Siku kama ya leo miaka 107 iliyopita, mfereji wa Suez uliokuwa ukidhibitiwa na Uingereza, ulishambuliwa na vikosi vya majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othmaniya katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Udhibiti wa mfereji huo wa Suez ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa pande mbili zilizokuwa zikipigana katika Vita vya Kwanza vya Dunia kutokana na ukweli kwamba mfereji huo ndio unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu. Uingereza ambayo haikuwa tayari kupoteza makoloni yake ya Asia, ilipigana vikali na majeshi ya Ujerumani na utawala wa Othomaniya na kupata ushindi. Mfereji wa Suez uliendelea kudhibitiwa na Uingereza hadi ulipotaifishwa na kiongozi wa Misri Gamal Abdul Nasir hapo mwaka 1956.

Mfereji wa Suez

Siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, Woodrow Wilson Rais wa 28 wa Marekani alifariki dunia. Woodrow Wilson alizaliwa 1913 na akiwa na umri wa miaka 57 alichukua hatamu za uongozi wa Marekani. Kama walivyokuwa marais waliomtangulia wa Marekani, na yeye alikita zaidi katika kuingilia masuala ya ndani ya Amerika ya Kati. Kipindi cha urais wa Woodrow Wilson kilitawaliwa na uingiliaji na uvamizi wa kijeshi dhidi ya maeneo mbalimbali duniani. Nusu ya kipindi cha utawala wa Woodrow Wilson, kilishuhudia Marekani ikishughulishwa na vita. Nchi zilizoshambuliwa kijeshi na Marekani katika uongozi wa Rais Woodrow Wilson ni Haiti, Guatemala, Dominican na Cuba.

Woodrow Wilson

Miaka 43 iliyopita katika siku kama leo, wakati wananchi wa Iran walipokuwa katika sherehe na shamrashamra za kurejea nchini Imam Khomeini akitokea uhamishoni nje ya nchi, Imam alizungumza na waandishi habari akieleza misimamo ya mfumo ujao wa utawala wa Kiislamu hapa nchini na kutangaza kuwa ataaunda serikali ya mpito ya mapinduzi muda mfupi baadaye. Imam Khomeini alitangaza kuwa serikali hiyo ya mpito itakuwa na jukumu la kutayarisha kura ya maoni ya Katiba mpya ya Iran. Vilevile alimtahadharisha Waziri Mkuu wa serikali ya wakati huo ya Shah kwamba, iwapo ataendelea kuwakandamiza wananchi angetangaza vita vya jihadi. Imam Khomeini vilevile alilitaka jeshi lijiunge na mapambano ya wananchi dhidi ya utawala wa Shah. Wakati huo pia ilitangazwa kwamba Wamarekani elfu 35 walikuwa wamekwishaondoka katika ardhi ya Iran na kwamba wengine elfu 10 wako mbioni kuondoka.

Imam Khomeini

Na siku kama ya leo miaka 12 iliyopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilirusha kwa mafanikio kombora la kwanza la kupeleka satalaiti angani la Omid. Miaka iliyofuata Iran ilituma viumbe hai angani kwa mafanikio ikiwa ni pamoja na kobe na tumbili na hatua hiyo iliingiaza Iran katika klabu ya nchi zenye teknolojia ya anga za mbali tena katika kipindi hicho cha vikwazo vikali vya kiuchumi vya nchi za Magharibi.