May 14, 2022 02:14 UTC
  • Jumamosi, 14 Mei, 2022

Leo ni Jumamosi tarehe 12 Mfunguo Mosi Shawwal 1443 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 14 Mei 2022 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 413 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, aliaga dunia alimu na mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahauddin Muhammad Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai. Sheikh Bahai ambaye alikuwa mtaalamu wa fiqhi, nujumu na hesabati alifariki dunia katika mji wa Isfahan nchini Iran. Alizaliwa mwaka 952 Hijria katika mji wa Baalabak huko Lebanon katika familia ya Kiirani. Baba yake alikuwa miongoni mwa mashekhe wakubwa wa zama hizo. Sheikh Bahai ameandika vitabu vingi ikiwa ni pamoja na Tashrihul Aflak, Kashkul na Hablul Matin. ***

Sheikh Bahauddin Muhammad Amili

 

Miaka 447 iliyopita katika siku kama ya leo, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno. Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuidhibiti nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kupigania uhuru wa nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru. ***

Angola

 

Siku kama ya leo miaka 226 iliyopita, chanjo ya kwanza kabisa ya ugonjwa wa ndui ilitolewa nchini Uingereza. Japokuwa hii leo ugonjwa huo umetoweka katika maeneo mengi ya dunia hususan katika nchi zilizoendelea, lakini hadi kufikia karne ya 18, maradhi hayo yalienea sana ndani ya mataifa mengi na kusababisha madhara makubwa. Mwaka 1717 mwanamke mmoja wa Uingereza alianzisha utafiti na uchunguzi mkubwa katika suala hilo, ambapo juhudi zake zilipunguza sana idadi ya waathirika wa maradhi hayo. Hatimaye tarehe 14 Mei mwaka 1796 Dakta Edward Jenner aliifanyia majaribio chanjo ya ndui kupitia mwili wa mtoto mdogo na kutoa majibu mazuri. ***

Ugonjwa wa ndui

 

Siku kama ya leo miaka 211 iliyopita, nchi ya Paraguay ilijipata uhuru wake. Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kulishudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyeingia madarakani aliongoza kidikteta. Uchaguzi wa kwanza huru wa rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia. ***

Bendera ya Paraguay

 

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 74, Joseph Reinaud, msomi na mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufarasa. Kutokana na kupendelea sana lugha za eneo la Mashariki ya Kati, alianza kujifunza lugha na fasihi ya Kiarabu. Baada ya muda mfupi, Joseph Reinaud alianza kufundisha lugha hiyo katika chuo kikuu nchini Ufaransa. Aliandika vitabu kuhusiana na historia ya Uislamu ambapo moja ya vitabu hivyo ni 'Fat'hul-Arab' na 'Al-Islamu wal-Muslimin.

Joseph Reinaud

 

Siku kama ya leo miaka 131 iliyopita, Ayatullah Mirza Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu, katika hatua ya kukabiliana na ukoloni wa Uingereza, alitoa fatwa ya kuharamisha utumiaji tumbaku nchini Iran. Katika kipindi cha utawala wa Nassir Deen Shah kutoka ukoo wa Qajaar Uingereza ilikuwa ikiongeza satwa yake nchini Iran kwa kufungua makampuni ya tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa imehodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini hapa. Fatua hiyo ilichukuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran. Kwa hakika fatwa hiyo iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni nchini. ***

Ayatullah Mirza Hassan Shirazi,

 

Katika siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, utawala bandia wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya Wapalestina. Askari wa Uingereza waliikalia kwa mabavu Palestina kufuatia kushindwa utawala wa Othmania wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Miaka mitano baadaye Jumuiya ya Kimataifa iliikabidhi Palestina kwa Uingereza na kuiweka chini ya mamlaka ya mkoloni huyo. Novemba mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ulipasisha azimio lililotaka kuundwa madola mawili ya Kiarabu na Kiyahudi katika ardhi ya Palestina. ***

Utawala wa Kizayuni

 

Na siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, mkataba wa kisiasa na kijeshi wa Warsaw ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw, lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya magharibi waitifaki wa Marekani. Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary. ***

Mkataba wa Warsaw

 

Tags