Nov 28, 2022 08:28 UTC
  • Shirika la Iran lapata zawadi ya D8 ya uhawilishaji wa teknolojia

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya taarifa katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Kampuni moja ya Iran ambayo msingi wake ni elimu au knowledge-based imeshinda tuzo ya mradi bora wa uhawilishaji wa teknolojia wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya D-8 ambayo inazileta pamoja nchi za Kiislamu zinazoendelea.

Tuzo ya mradi wa uhawilishaji wa teknolojia kati ya makampuni manane ya nchi zinazoendelea za Kiislamu inayojulikana kama Kitengo cha Ushirikiano wa Kiuchumi cha D-8 huko Ankara, mji mkuu wa Uturuki lilikabidhiwa kwa pamoja kwa kampuni ya ujuzi ya Iran inayozalisha mashine na nanofibers na kampuni nyingine ya Malaysia.

Mkuu wa Kituo cha Maendeleo ya Teknolojia cha Iran, Milad Sardkhanlou ameashiria kuundwa kwa mtandao wa kubadilishana teknolojia kwa lengo la kuendeleza ushirikiano wa kiteknolojia kati ya nchi nane za Kiislamu na kueleza kuwa sekretarieti ya mtandao huu ilianzishwa nchini Iran katika Bustani ya Teknolojia ya Pardis. Amesema lengo kuu la sekretarieti hii ni kukusanya na kutathmini mipango ya kiteknolojia ya nchi za Kiislamu.

Alibainisha kuwa madhumuni ya kutoa tuzo ya mpango bora wa uhamishaji wa teknolojia ni kuendeleza ushirikiano wa kiteknolojia kati ya nchi za D-8 na kusaidia kampuni za kibinafsi zinazozingatia maarifa.

Mkuu wa Shirika la Sayansi na Teknolojia la Turkiye, Hasan Mandal amesema maendeleo ya miradi ya teknolojia ya nchi za Kiislamu ni ya kuvutia.

Ameelezea matumaini kuwa miradi ya teknolojia iliyopendekezwa ya nchi zinazoendelea za Kiislamu itaongezeka zaidi.

Shirikisho la watengeza magari barani Ulaya limeitangaza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa taifa la kumi duniani kwa kuzalisha na kutengeneza magari madogo.

Shirikisho la watengeza magari barani Ulaya limeitangaza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa taifa la kumi duniani kwa kuzalisha na kutengeneza magari madogo.

Taarifa ya shirikisho hilo imeeleza kuwa, katika kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu, Iran ilizalisha magari mengi madogo na kuyapiku mataifa makubwa kama Ufaransa, Uingereza na Italia nukta inayoashiria kuwa Iran imepiga hatua katika uga wa teknolojia ya kuunda magari ya kiwango cha juu na kwa teknolojia ya kisasa duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya sekta ya viwanda, katika kipindi cha kati ya Januari na Septemba mwaka huu jumla ya magari  49,817,000 yalitengenezwa na kuzalishwa duniani ambapo hisa ya Iran ilikuwa asilimia 1.9 na kuifanya ishike nafasi ya kumi duniani kwa kutengeneza magari madogo.

Katika mwaka uliopita na katika kipindi cha Januari hadi Septemba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilishika nafasi ya 13 duniani kwa kuzalisha magari madogo. Hili ni ongezeko la asilimia 31.2 ikilinganishwa na mwaka jana.

Chama cha watengezaji magari barani Ulaya kimesema kuwa, mwaka huu hadi kufikia mwezi Septemba, Iran imeyapiku mataifa mengi katika kuzalisha magari madogo duniani kama Russia, Jamhuri ya Czech na Slovakia.

Kiwanda cha Magari Iran

Aidha mataifa makubwa ya Ulaya kama Ufaransa, Uingereza na Italia yameachwa nyuma na Iran katika miezi tisa ya awali ya mwaka huu katika uga wa utengenezaji magari madogo.

Katika kipindi hiki Iran imeweza kutengeneza magari madogo ya kutembelea 949,726 huku Ufaransa ikitengeneza magari 693,000.

Jamhuri ya Kiislamu imeendelea kupiga hatua za ustawi na maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya utengezaji magari na kuongeza kiwango cha uzalishaji licha ya kuandamwa na vikwazo vya kiuchumi na mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ya Marekani na washirika wake.

@@@

Kongamano la kimataifa la wataalamu wa ugonjwa wa kifua kikuu au TB limefanyika hivi karibuni mjini Nairobi Kenya kujadili mbinu mujarabu za kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta za umma kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa huo hatari huku apu ya t-bu Lite ikitajwa kuleta mapinduzi katika tiba.

Kifua kikuu husambazwa kupitia hewa pale mtu anapovuta hewa iliyo na bakteria aina ya Mycobacterium tuberculosis wakati wa kukohoa.

Kwa mujibi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO, TB ni moja ya magonjwa 10 yanayosababisha vifo vingi duniani. Kwa kiasi kikubwa kifua kikuu huathiri mapafu lakini sehemu nyingine mwilini pia zinaweza kuambukizwa. 

Takwimu za WHO zinaonyesha kuwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa kifua kikuu duniani ni watu wazima na wengi wao ni wanaume. WHO imeiondoa Kenya na mataifa mengine 5 kwenye orodha ya mataifa 30 yaliyo na visa vingi vya wagonjwa wa kifua kikuu duniani.

WHO kwenye taarifa yake ya mwaka wa 2022 imeelezea kuwa kwa mataifa mengine, hali ilikuwa mbaya zaidi ukizingatia athari za janga la corona au COVID-19. 

Mary Nzamalu ni afisa wa matibabu na msimamizi wa mpango wa kifua kikuu kwenye kaunti ya Nairobi anafafanua kuwa,”Kwa sasa wagonjwa wakija wanapimwa COVID 19 na kifua kikuu kwa pamoja maana dalili zinafanana. Idadi ya walioambukizwa imeongezeka kwa sababu waliokuwa hawawezi kufika hospitalini kwa sababu ya vikwazo vya corona sasa wana uhuru wa kutembea na wanapata huduma.”

Kwenye taarifa yake, shirika la WHO, linasisitiza umuhimu wa kutengwa fedha zaidi za kupambana na kifua kikuu haraka iwezekanavyo ukizingatia madhila ya janga la COVID 19. 

Mwaka 2021 watu milioni 10.6 waliugua kifua kikuu, idadi ambayo ni ongezeko la asilimia  4.5% kutokea mwaka ulopita wa 2020. 

Ripoti ya WHO inabainisha kuwa watu milioni 1.6 walikufa kutokana na kifua kikuu au TB katika kipindi hicho. Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka kadhaa, idadi ya wanaougua kifua kikuu na kifua kikuu sugu imeongezeka. Kwa mujibu wa WHO idadi ya maambukizi mapya ya kifua kikuu sugu iliongezeka kati ya mwaka 2020 na 2021.

Kwa mantiki hiyo shirika hilo la afya linasema, idadi kubwa ya walioambukizwa kifua kikuu hawakupimwa wala kutibiwa. 

Mike Macharia ni Meneja wa kiufundi katika mpango wa Komesha TB nchini Kenya anaelezea umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika vita dhidi ya kifua kikuu na kusisitiza kuwa,”Apu hii  t-bu Lite inamuwezesha mhudumu wa afya kumsajili mgonjwa, kunakili maelezo yake, kuhifadhi takwimu na kumwelekeza kwenye kituo cha afya kilicho karibu naye kokote ndani ya mipaka ya Kenya. Hii ina maana hata pale anapohamia sehemu nyingine bado maelezo yapo na wataalamu wa afya wana uwezo wa kuarifiwa anapotokea mgonjwa wa kifua Kikuu.”

Apu ya t-bu Lite imeleta tija hasa katika kuhifadhi takwimu na ufuatiliaji wa wagonjwa wa Kifua Kikuu kokote waliko ndani ya mipaka ya Kenya. 

Takwimu zinaashiria kuwa mwaka 2021 idadi ya maambukizi ya Kifua kikuu yalipungua ila bado hayakufikia viwango vya kabla ya janga la corona kuzuka.

Hali kwamba idadi ya walioambukizwa TB imepungua inaashiria kuwa ambao hawajapimwa na kutibiwa wameongezeka na hatimaye kusababisha ongezeko la vifo. 

Shirika la afya linasema hii ina maana kuwa baada ya muda idadi ya walioambukizwa Kifua Kikuu itaongezeka.

Naam na hadi hapo ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya sayansi, tiba na teknolojia....