Jun 23, 2016 06:07 UTC
  • Alkhamisi 23 Juni, 2016

Leo ni Alkhamisi tarehe 17 Ramadhani 1437 Hijria inayosadifiana na tarehe 23 Juni 2016.

Siku kama ya leo miaka 1438 iliyopita kwa mujibu wa baadhi ya nukuu za historia Mtume Mtukufu Muhammad SAW alisafiri kutoka Makka hadi Baitul Muqaddas na kupaa mbinguni kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Aya ya kwanza ya Sura ya al Isra inatoa maelezo kuhusu muujiza huo mkubwa ikisema. "Ametakasika aliyemchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyouzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara Zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Kwenye kuona." Kwa kuzingatia aya hiyo na hadithi za Mtume Muhammad SAW, wakati mtukufu huyo alipokuwa katika safari ya Miiraji alionyeshwa siri nyingi za Mwenyezi Mungu SW, viumbe vyake Jalali na hatima ya wanadamu katika ulimwengu wa Akhera.

Tukio hilo ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume Muhammad SAW na linadhihirisha nafasi ya juu ya mtukufu huyo.

Tarehe 17 Ramadhani miaka 1435 iliyopita, vita vya Badr, moja kati ya vita maarufu vya Mtume Muhammad SAW, vilitokea katika eneo lililoko kati ya Makka na Madina. Badr ni jina la kisima kilichoko umbali wa kilomita 120 kusini magharibi mwa mji wa Madina, ambako kulipiganwa vita vya kwanza kati ya Waislamu na washirikina. Vita vya Badr vilitokea huku washirikina wakiwa na wapiganaji wengi waliokaribia 920 na jeshi la Kiislamu likiwa na wapiganaji 313 na silaha chache. Hata hivyo imani thabiti ya Waislamu iliwafanya washinde vita hivyo.

Siku ya leo miaka 480 iliyopita, ilianza harakati ya kiongozi wa kidini na mpenda mageuzi wa Ufaransa Calvin John huko Geneva mji mkuu wa Uswisi. Alizaliwa mwaka 1509 Miladia na kujifunza sheria na masomo ya kidini. Katika zama za ujana wake, Calvin John alijiunga na harakati ya Kiprotestanti ilioasisiwa na Martin Luther. Aliivamia Geneva Uswisi kwa kusaidiwa na wafuasi wa Kiprotestanti na kujaribu kuasisi mfumo wa uongozi wa kidini katika jamii ya nchi hiyo kwa mujibu wa dhehebu la Protestanti. Calvin John pia alianzisha mfumo wa ideolojia ya Kikristo iliyojulikana kama Calvinism na kubainisha itikadi zake katika kitabu chake alichokiita" Institutes of Christian Religion."

Miaka 259 iliyopita na katika siku muwafaka na leo, vilijiri vita vya kwanza kati ya vikosi vya Uingereza na India huko katika eneo la Bengali kaskazini mashariki mwa India. Waingereza walishinda vita hivyo na kulidhibiti eneo hilo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya India. Waingereza ambao walianza kuingia nchini India miaka kadhaa nyuma kupitia East Indian Company, mbali na kuyarejesha nyuma majeshi ya India, katika vita vilivyofuata ilimshinda pia hasimu wake mkubwa Ufaransa na kufanikiwa kuyatoa kabisa majeshi hayo katika ardhi ya India.

Na tarehe 24 Juni miaka 76 iliyopita, Wafaransa waliikabidhi rasmi Uturuki bandari muhimu ya Iskenderun, eneo ambalo katika zama hizo lilikuwa sehemu ya ardhi ya Syria. Kwa miaka kadhaa kabla ya tukio hilo, Uturuki ilikuwa ikidai umiliki wa bandari hiyo. Hata hivyo baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia, eneo hilo lilikabidhiwa Syria kwa mujibu wa makubaliano yaliyokuwa yamefikiwa baina ya Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo baada ya kuangushwa utawala wa Othmania na kuchukua hatamu za uongozi nchini Uturuki, Mustafa Kamal Ataturk aliyekuwa na mielekeo ya Kimagharibi Ufaransa ambayo wakati huo ilikuwa ikiikalia kwa mabavu Syria, iliikabidhi Bandari ya Iskenderun kwa Uturuki. Hatua hiyo ilipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya Ufaransa nchini Syria na kusababisha mapambano dhidi ya mkoloni huyo kuongezeka. Hadi leo hii serikali ya Syria ingali inasisitiza kwamba, Bandari ya Iskenderun ni mali yake.