May 24, 2023 17:21 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 917 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 45 ya Al-Jaathiya. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 15 ya sura hiyo ambayo inasema:

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا فَلِنَفْسِهِ ۖ وَمَنْ أَسَاءَ فَعَلَيْهَا ۖ ثُمَّ إِلَىٰ رَبِّكُمْ تُرْجَعُونَ

Anayetenda mema basi anajitendea mwenyewe, na mwenye kufanya uovu ni juu yake mwenyewe. Kisha mtarudishwa kwa Mola wenu Mlezi.

Aya ya mwisho tuliyosoma katika darsa iliyopita ilizungumzia namna ya kuamiliana na watu wanaokanusha Kiyama. Aya hii ya 15 inasema: msidhani kama kuamini na kukufuru kwenu, au kutii na kuasi kwenu kuna faida au hasara yoyote kwa Mwenyezi Mungu. Chochote kifanywacho na yeyote yule, matokeo yake yatamrejea mfanyaji wake na atapata Siku ya Kiyama malipo ya hicho alichokifanya. Ni sawa kabisa kama mwalimu anavyomweleza mwanafunzi wake kwamba: ukisoma au usisome masomo yako, faida na hasara itakayopatikana itakurejea wewe mwenyewe; mimi sipati manufaa au madhara yoyote yale. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, mfumo wa Allah SWT wa jaza na malipo kwa waja unatokana na amali njema au mbaya wanazofanya; na wanadamu wote wako sawa mbele ya sheria za Mwenyezi Mungu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu si mhitaji kwa mwanadamu; na yanachofanya hasa mafundisho ya dini ni kumlea na kumjenga mtu ili afikie kwenye utukukaji na ukamilifu wa kiutu.

Zifuatazo sasa ni aya ya 16 na 17 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ آتَيْنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ الْكِتَابَ وَالْحُكْمَ وَالنُّبُوَّةَ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ

Na kwa hakika tuliwapa Wana wa Israili Kitabu na hukumu na Unabii, na tukawaruzuku vitu vizuri vizuri, na tukawafadhilisha kuliko walimwengu wote (wa zama zao). 

وَآتَيْنَاهُم بَيِّنَاتٍ مِّنَ الْأَمْرِ ۖ فَمَا اخْتَلَفُوا إِلَّا مِن بَعْدِ مَا جَاءَهُمُ الْعِلْمُ بَغْيًا بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّ رَبَّكَ يَقْضِي بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ

Na tukawapa maelezo wazi ya amri. Basi hawakukhitalifiana ila baada ya kuwafikia ilimu, kwa uhasidi uliokuwa baina yao. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika mambo waliyo kuwa wakikhitalifiana. 

Aya hizi zinaashiria neema kubwa ambazo Mwenyezi Mungu aliipa kaumu ya Bani Israil huko nyuma, ili jambo hilo liupe ibra na mazingatio umma wa Uislamu. Kwanza aya zimeashiria neema ya Kitabu cha mbinguni, kuweza kuasisi utawala na kupelekewa Mitume; na kisha zinaashiria riziki safi walizoteremshiwa watu wa kaumu hiyo na kusema: kwa sababu ya neema na atiya hizo, walikuwa na hadhi ya juu zaidi katika walimwengu wa zama zao. Lakini kwa masikitiko, walihitilafiana na kufarikiana kutokana na uhasidi na ushindani uliozuka baina yao. Japokuwa walidhihirikiwa na haki kwa uwazi kabisa na zilikuwepo hoja za kutosha kulingana na kitabu cha mbinguni walichoteremshiwa, za kuwafanya waufahamu ukweli, lakini hawakuacha kuhitilafiana. Waliendeleza hitilafu na mifarakano baina yao mpaka wakapoteza nguvu na adhama waliyokuwa nayo pamoja na utawala wao. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, neema zote tulizonazo; za kimaada, yaani za vitu; na za kimaanawi, yaani za mafanikio kiroho na kidini, tujue kwamba zimetokana na Mwenyezi Mungu; na tuzitumie kwa usahihi ili tupate hadhi ya juu hata hapa duniani. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, hakuna mgongano kati ya unabii na utawala; na kimsingi hasa ni kwamba, siasa inatakiwa iendeshwe kwa kufuata misingi na thamani za kidini. Halikadhalika, aya hizi zinatuelimisha kwamba, Mwenyezi Mungu ametimiza dhima kwa watu na kuwawekea hoja za wazi kabisa za kufahamu haki na ukweli; kwa hivyo hawatakuwa na kisingizio cha kuwafanya wasisailiwe na kuwajibishwa Siku ya Kiyama. Wa aidha aya hizi zinatutaka tujue kuwa, kujua na kufahamu peke yake hakutoshi; kwani si hasha mtu akawa na uelewa wa haki, lakini kutokana na inadi na ukaidi wa nafsi au uhasidi akaikataa haki na kueneza hitilafu na mifarakano ndani ya jamii.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 18 hadi 20 za sura yetu ya al Jaathiya ambazo zinasema:

‏ ثُمَّ جَعَلْنَاكَ عَلَىٰ شَرِيعَةٍ مِّنَ الْأَمْرِ فَاتَّبِعْهَا وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَ الَّذِينَ لَا يَعْلَمُونَ

Kisha tukakuweka wewe juu ya Sharia katika amri, basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wale wasio jua (kitu).

إِنَّهُمْ لَن يُغْنُوا عَنكَ مِنَ اللَّهِ شَيْئًا ۚ وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۖ وَاللَّهُ وَلِيُّ الْمُتَّقِينَ

Kwa hakika hao hawatakufaa chochote mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao. 

هَٰذَا بَصَائِرُ لِلنَّاسِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُوقِنُونَ

Hizi ni dalili zilizo wazi kwa watu (wote), na ni uwongofu, na rehema kwa watu wanao yakinisha.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia habari za kaumu ya Bani Israil, aya tulizosoma zinamhutubu Bwana Mtume Muhammad SAW ya kwamba: sisi tumekuwekea na wewe pia sharia na mwongozo wa wazi wa kukuelekeza kwenye dini ya haki, ili kwa dini hiyo uwalinganie watu imani ya tauhidi ya kumwabudu Mungu mmoja na pekee wa haki. Kwa kufanya hivyo, bila ya shaka washirikina na wapinzani watasimama kukabiliana na wewe na hata kutaka kukupa mapendekezo kadhaa kwa lengo la kuzuia dini yako isienee. Lakini usikubali katu kufanya mapatano na maridhiano nao kuhusu dini ya Mwenyezi Mungu. Ewe Mtume, simama imara na kwa uthabiti katika njia ya haki na shikamana nayo barabara. Fuata amri za Mwenyezi Mung tu, wala usikubali na wala usiyajali katu matakwa ya wapinzani. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawasimamia na kuwaongoa wale wanaomcha Yeye tu. Lakini kwa wale makafiri walio madhalimu, wao ni washirika na wasaidizi wa wenzao walio mfano wao; na hawana uwezo wa kumdhuru mtu au kumnusuru na kumuokoa na adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hii Qur'ani uliyoteremshiwa wewe inatosha kwa watu wote; kwa sababu ni wenzo wa kuonea watu wote na dira ya kupatia uono sahihi kwa pande zote za maisha. Hapana shaka kuwa, yeyote anayetaka kufikia marhala na hatua ya kupata yakini, kitabu hiki kitamwongoza na kumwezesha kupata rehma maalumu za Allah. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kila moja kati ya dini za tauhidi ina njia yake ya kumfikisha mtu kwenye haki na ukweli, lakini zote zinatokana na chimbuko na asili moja. Dini ya mwisho ya Uislamu imekuja kuendeleza dini ileile ya tauhidi waliyokuja kuilingania Mitume waliotangulia. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mtu asiye tayari kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, hulazimika kufuata hawaa na matamanio ya nafsi yake au ya watu wengine ambayo hayatokani na uelewa, ujuzi na ufahamu sahihi wa ukweli na haki. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, kufuata matakwa yasiyo na maana ya watu majahili ni sawa na kukubali kuwa chini ya mamlaka yao na kujiweka mbali na mamlaka ya Mwenyezi Mungu. Wa aidha aya hizi zinatutaka tuelewe kuwa, ufuataji dini inapasa utokane na basira, ujuzi na uelewa ili uweze kumwongoza mtu na kumfikisha kwenye hakika na yakini. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, Qur'ani ni dira inayoongoza na kutoa mwanga katika nyuga zote za kifikra, kiakhlaqi, kijamii, kisiasa na kifamilia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 917 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/