Sura ya Muhammad, aya ya 7-14 (Darsa ya 929)
Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.
Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 929 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya saba hadi ya tisa za sura hiyo ambazo zinasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَنصُرُوا اللَّهَ يَنصُرْكُمْ وَيُثَبِّتْ أَقْدَامَكُمْ
Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu.
وَالَّذِينَ كَفَرُوا فَتَعْسًا لَّهُمْ وَأَضَلَّ أَعْمَالَهُمْ
Na walio kufuru, basi kwao ni maangamizo, na atavipuuza vitendo vyao.
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَرِهُوا مَا أَنزَلَ اللَّهُ فَأَحْبَطَ أَعْمَالَهُمْ
Hayo ni kwa sababu waliyachukia aliyo yateremsha Mwenyezi Mungu, basi akaviangusha vitendo vyao.
Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia namna ya kukabiliana na maadui wa Uislamu katika medani ya vita. Aya tulizosoma zinaendeleza maudhui hiyo kwa kuwahutubu waumini ya kwamba: medani ya vita ni uwanja wa mapambano na mapigano na ina taabu na misukosuko yake maalumu. Kwa hivyo inapasa muwe na subira na istiqama katika njia hiyo ya kulinda dini na ardhi yenu na wala msikimbie katika uwanja wa jihadi. Kama mtakuwa thabiti mbele ya maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu, kuweni na uhakika kwamba na Yeye Allah SWT atakupeni auni na msaada na mtamshinda adui yenu. Na sababu ni kuwa Yeye Mola ameshahukumu maadui hao wasambaratike na kuangamia na kwa hivyo ataizima na kuishinda mipango na njama zao. Lakini wao maadui, badala ya kujisalimisha mbele ya mafundisho yenye kuhuisha roho, ya Allah na Mtume wake, wameamua kukabiliana nayo kwa vita. Kwa sababu hiyo, hawatakuwa na hatima nyingine ila kuharibikiwa na kuangamia; na hayo wayafanyayo hayatawawezesha kupata wanayoyadhamiria. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kuamini tu peke yake hakutoshi; inapasa mtu afanye juhudi na bidii pia za kuitangaza na kuieneza dini ya Mwenyezi Mungu na kupambana na wale wanaoifanya jamii ipotoke kwa kuacha mkondo na njia ya dini. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, njia na namna ya kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu huwa inatafautiana katika kila zama kulingana na hali na mazingira. Kuna wakati huwa ni kwa kufanya tablighi na kutangaza mafundisho yake, kuna wakati huwa ni kwa njia ya kutoa na kusaidia kifedha na wakati mwingine hulazimu mtu kujitoa mhanga na kusabilia roho na maisha yake kwa ajili ya kuinusuru dini ya Allah. Halikadhalika aya hizi zinatuelimisha kwamba, kuyachukia moyoni mafundisho ya dini ni alama ya aina mojawapo ya ukafiri uliomo ndani ya nafsi ya mtu, ambao hupelekea kuporomoka na kutoweka amali zake njema. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hizi kuwa, kuipiga vita haki hakuna mwisho mwingine isipokuwa kuharibikiwa na kumfanya mtu aporomoke na kuangukia kwenye lindi la maangamizi maishani.
Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 10 na 11 za sura yetu ya Muhammad ambazo zinasema:
أَفَلَمْ يَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ دَمَّرَ اللَّهُ عَلَيْهِمْ ۖ وَلِلْكَافِرِينَ أَمْثَالُهَا
Kwani hawakutembea katika ardhi wakaona ulikuwaje mwisho wa walio kuwa kabla yao? Mwenyezi Mungu aliwaangamiza, na kwa makafiri hawa itakuwa mfano wa hayo.
ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّهَ مَوْلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَأَنَّ الْكَافِرِينَ لَا مَوْلَىٰ لَهُمْ
Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ni Msimamizi (na msaidizi) wa walio amini. Na makafiri hawana msimamizi (na msaidizi).
Katika mwendelezo wa yaliyoelezwa katika aya zilizotangulia, katika aya hizi, Allah SWT anawapa indhari makafiri na washirikina waliokuwa wakiwafanyia uadui Waislamu ya kwamba, mkisafiri na kutupia jicho maeneo ya kandokando yenu mtayaona magofu na athari zilizoachwa na watu wa kaumu zilizopita, namna gani walivyoangamizwa na hivi sasa hayatajwi tena majina wala kumbukumbu zao. Kwa hiyo msidhani kama hatima kama hiyo iliwahusu wao tu na wala haikujumuisheni nyinyi. Tambueni kuwa kama na nyinyi pia mtafuata njia waliyofuata wao, mtafikwa na hatima hiyohiyo na mtaangamia. Hakika ni kwamba, hakuna yeyote wa kukusaidieni na kukuokoeni, kwa sababu Mwenyezi Mungu hawapi nusra wala msaada maadui zake. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kutalii na kusoma historia ya waliotangulia na kujionea kwa karibu ardhi walizokuwa wakiishi ni miongoni mwa malengo ya safari, matembezi na utalii katika Uislamu na kwa ajili ya kupata ibra na mazingatio juu ya hatima iliyowafika watu wa kaumu zilizopita. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, yasituhadae madhihirisho ya raha na starehe tunayoyaona hivi sasa kwa makafiri, kwani watu hao hawatakuwa na hatima na mwisho mwema. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, kumwamini Mwenyezi Mungu ni njia ya kupatia rehma na msaada wa Mola duniani na akhera; na kumkufuru, ndio sababu ya mja kuyakosa hayo.
Ifuatayo sasa ni aya ya 12 ambayo inasema:
إِنَّ اللَّهَ يُدْخِلُ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ وَالَّذِينَ كَفَرُوا يَتَمَتَّعُونَ وَيَأْكُلُونَ كَمَا تَأْكُلُ الْأَنْعَامُ وَالنَّارُ مَثْوًى لَّهُمْ
Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walio amini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito chini yake. Na walio kufuru hujifurahisha na hula kama walavyo wanyama, na Moto ndio makaazi yao.
Baada ya kulinganishwa waumini na makafiri walivyo hapa duniani, aya hii inalinganisha hali na daraja zao Siku ya Kiyama na kueleza kwamba, waumini, ambao walitekeleza sawasawa wajibu na majukumu yao hapa duniani na wakajitahidi kufanya mambo mema na ya kheri, Siku ya Kiyama watakuwa katika raha na furaha kwa kuwekwa kwenye makazi yenye kila aina ya neema. Lakini makazi ya walioipiga vita haki yatakuwa ni kwenye Moto uteketezao. Sababu ni kuwa, wao walijali raha na starehe za kupita za dunia, kwa kufikiria matumbo, shahawa na matamanio yao tu mithili ya nyamahoa; na wala hawakushughulika kujiandalia masurufu yoyote kwa ajili ya safari ya akhera. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, utumiaji wa raha na starehe za dunia hii, uwe ni mwingi au mchache una mwisho na ni wa muda mfupi tu, kwa hivyo tufikirie masurufu ya akhera ambako kutabaki na kudumu milele. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Qur'ani inajuzisha mwandamu kuburudika na neema za dunia, lakini si kwa kiumbe huyo aliyetukuzwa na Allah kuishi maisha kama ya mnyama. Halikadhlika tunajielimisha kutokana na aya hii kwamba, katika kuchagua njia ya maisha, tuzingatie itakavyokuwa hatima na mwisho wake, si kutekwa na mapambo yake ya njiani tu tunayoyapita haraka na kuyaacha nyuma.
Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 13 na 14 ambazo zinasema:
وَكَأَيِّن مِّن قَرْيَةٍ هِيَ أَشَدُّ قُوَّةً مِّن قَرْيَتِكَ الَّتِي أَخْرَجَتْكَ أَهْلَكْنَاهُمْ فَلَا نَاصِرَ لَهُمْ
Na miji mingapi iliyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mji wako huu ulio kutoa; nao tuliwateketeza na wala hawakuwa na wa kuwanusuru.
أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ كَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ وَاتَّبَعُوا أَهْوَاءَهُم
Je! Mwenye kuwa na hoja ya wazi kutoka kwa Mola wake Mlezi atakuwa sawa na aliye pambiwa uovu wa vitendo vyake, na wakafuata matamanio ya nafsi zao?
Aya hizi zinazungumzia sifa mbaya na chafu za makafiri na kueleza kwamba, wao wanajivunia nguvu za mamlaka na utajiri wao wa mali; na wanadhani kuwa hakuna yeyote awezaye kukabiliana na wao. Hali ya kuwa hatima za kaumu zilizopita zinaonyesha kuwa, watu wake waliangamizwa kwa irada ya Allah SWT na hakuna mtu yeyote aliyeweza kuwasaidia na kuwaokoa. Sifa nyingine mbaya ya makafiri ni kwamba wametekwa na kughilibiwa na hawaa na matamanio ya nafsi na kujali yenye manufaa na wao tu mpaka wamefika hadi ya kuyaona machafu na maovu yao ni mambo safi na mazuri. Na kwa hivyo yale ya haki yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu wanayaona mabaya na hawako tayari kuyafuata. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, waumini wasiuhofu uwezo na nguvu za kidhahiri za maadui wa Allah, kwa sababu nguvu na uwezo wa Mola uko juu ya nguvu na uwezo wote wa wanadamu. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, maadui wanabuni na kutumia njia na mbinu za kuwataabisha na kuwaudhi waumini, lakini waumini wa kweli katu hawatetereki katika imani yao na wanaendeleza juhudi na mapambano yao. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, imani imejengeka juu ya misingi ya hoja na burhani, lakini ukafiri umesimama juu ya dhana hewa na potofu na hawaa na matamanio ya nafsi. Aya hizi zinatutaka tuelewe pia kuwa, kwa kutumia fitra na maumbile aliyopewa na Allah, mwanadamu anaufahamu ubaya wa matendo yake, lakini huufifisha kwa sababu ya matakwa na matashi ya nafsi yake na kutumia njia tofauti ili kuyafanya mabaya yake yaonekane mazuri na ya kupendeza. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 929 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/