May 27, 2023 04:19 UTC
  • Sura ya Muhammad, aya ya 18-20 (Darsa ya 931)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 931 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 18 ya sura hiyo ambayo inasema:

فَهَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا السَّاعَةَ أَن تَأْتِيَهُم بَغْتَةً ۖ فَقَدْ جَاءَ أَشْرَاطُهَا ۚ فَأَنَّىٰ لَهُمْ إِذَا جَاءَتْهُمْ ذِكْرَاهُمْ

Kwani wanangojea jengine isipo kuwa iwafikie Saa (ya Kiyama) kwa ghafla? Na hakika alama zake zimekwisha kuja. Na itapo wajia kutawafaa wapi kukumbuka kwao? 

Katika darsa iliyopita tulisoma aya iliyozungumzia watu wakaidi na wenye inadi, ambao walikuwa wakiamiliana na Bwana Mtume SAW kwa kejeli na stihzai. Aya tuliyosoma inazungumzia watu wanaokanusha kufufuliwa, yaani Maadi ambao wanasema: hatuamini Kiyama mpaka tukishuhudie kwa macho yetu; hali ya kuwa kuna hoja na ishara za wazi kabisa za kuthibitisha uwezekano wa kutokea kwake. Ikiwa watu hao wana nia ya kweli ya kuikubali haki, watakiamini Kiyama na kufufuliwa viumbe kwa hoja za kimantiki tu zilizopo kabla ya kukiona kwa macho yao. Na kama hawaliamini hilo hivi sasa, wakati watakapokuja kukiona kwa macho yao, kuamini kwao wakati huo hakutakuwa na faida yoyote tena kwao. Ni sawa kabisa na mgonjwa aliyekwenda kwa tabibu, ambaye baada ya kumpima akabaini maradhi yake akamwandikia dawa za kumtibu, lakini akazikataa kwa kusema: mimi siamini kama nina maradhi na wala siko tayari kutumia dawa mpaka niyahisi hayo maradhi yanataka kuniua. Ni wazi kwamba ifikiapo hatua hiyo, dawa na matibabu hayatakuwa na faida yoyote kwa mtu huyo na wala majuto na masikitiko hayatamfalia kitu mgonjwa huyo. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, makafiri na wakanushaji wa kufufuliwa viumbe wanaacha kuitumia fursa waliyopewa kutubia na kuomba maghufira kutokana na inadi na ukaidi wao; na kwa hakika wanaupoteza bure muhula waliopewa na Allah SWT. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, kuna hoja na ishara nyingi sana za kuthibitisha kuwa Kiyama kitajiri, lakini hoja na ishara hizo hazimthibitikii kila mtu, isipokuwa yule mwenye masikio ya kusikiliza na moyo wa kuikubali haki.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 19 ambayo inasema:

فَاعْلَمْ أَنَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا اللَّهُ وَاسْتَغْفِرْ لِذَنبِكَ وَلِلْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ ۗ وَاللَّهُ يَعْلَمُ مُتَقَلَّبَكُمْ وَمَثْوَاكُمْ

Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu, na omba maghufira kwa dhambi zako na za Waumini wanaume na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu anajua mahali penu pa kwenda na kurudi, na mahali penu pa kukaa. 

Baada ya aya iliyotangulia kuashiria inadi na ukaidi wa makafiri, aya hii inamhutubu Bwana Mtume SAW ya kwamba, wewe kwa upande wako simama imara na kuwa thabiti katika njia unayofuata, na ujue kwamba, ghairi ya Mwenyezi Mungu, Mola mmoja na pekee, hakuna nguvu nyingine yoyote iliyo na uwezo wa kufanya kitu katika dunia hii, na hakuna yeyote awezaye kumshinda Yeye Allah SWT. Kwa hivyo katika kila hali, tawakal, mtegemee na omba hifadhi kwake Yeye tu na wala usihofu wingi wa maadui wanaokukabili. Kisha aya inaendelea kutilia mkazo nukta moja ya msingi, nayo ni kwamba, waumini wanatakiwa wachunge taqwa na kumcha Mola wao; na kama watateleza na kukosea kwa lolote lile wamuombe maghufira na msamaha Yeye Allah SWT. Na yeye Bwana Mtume Muhammad SAW ni mwenye kujiombea maghufira yeye mwenyewe na kuwaombea waumini pia. Lakini kama tujuavyo, na ni wazi kwamba Mitume ni waja waliotakasika na madhambi; na madhumuni ya kuambiwa Mtume SAW aombe maghufira si kusamehewa madhambi, bali ni kudhihirisha moyo wa khushuu, udhalili na unyenyekevu mbele ya Muumba, kwa maana ya kujihisi muda wote kuwa yeye ni mkosa tu mbele ya Mola wake. Na sababu ni kwamba, jukumu la kufikisha risala na ujumbe wa Allah ni masuulia na mzigo mzito ambao Yeye Mola amewabebesha Mitume wake. Na kutokana na taqwa, khushuu na unyenyekevu walionao, huwa daima wanajihisi hawajaweza kutekeleza vile inavyostahiki hasa jukumu na masuulia hayo waliyonayo, jambo ambalo huwafanya wawe na hima na bidii kubwa zaidi na zaidi katika utekelezaji na kutotosheka wala kuridhishwa na idili na jitihada zozote zile wanazofanya. Tunaposoma aya mbalimali za Qur'ani tukufu inatubainikia kuwa si kuhusiana na Bwana Mtume SAW peke yake, bali aya hizo za kitabu hicho kitukufu zimezungumzia pia Mitume wengine waliotangulia, walioomba msamaha na maghufira kwa Allah SWT. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, maneno, mwenendo na matendo yetu yote yanatakiwa yasimame juu ya msingi wa Tauhidi na imani ya Mungu mmoja na pekee wa haki. Kufanya hivyo kutatuvua na utegemezi wa nguvu na uwezo hewa wa binadamu wenzetu na wala hatutakuwa na woga au hofu yoyote juu ya nguvu hizo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, wanaume na wanawake walioamini kikweli watakuwa kwenye kundi la watakaoombewa maghufira na msamaha na Mtume wa Mwenyezi Mungu, ambaye mbali na kuwaelekeza watu kwenye uongofu, anawaombea pia kwa Mola wawe na uzima, usafi na utoharifu wa roho na nafsi. Halikadhalika aya hii inatutake tufahamu kwamba, Mitume, kama walivyo watu wengine, nao pia ni binadamu, na kwa hivyo maumbile yao yanafungamana na hali na mazingira ya kibinadamu. Kwa hivyo, na wao pia wanahitaji rehma na uraufu wa Mola ili kufidia mipaka na nyudhuru za kibinadamu walizonazo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 20 ya sura yetu ya Muhammad ambayo inasema:

وَيَقُولُ الَّذِينَ آمَنُوا لَوْلَا نُزِّلَتْ سُورَةٌ ۖ فَإِذَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ مُّحْكَمَةٌ وَذُكِرَ فِيهَا الْقِتَالُ ۙ رَأَيْتَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ نَظَرَ الْمَغْشِيِّ عَلَيْهِ مِنَ الْمَوْتِ ۖ فَأَوْلَىٰ لَهُمْ

Na Waumini wanasema: Kwa nini haiteremshwi Sura? Na inapo teremshwa Sura iliyo waziwazi na ikatajwa ndani yake khabari ya vita, utawaona wenye maradhi katika nyoyo zao wanakutazama mtazamo wa anaye zimia kwa mauti. Basi (hayo mauti) ni bora kwao.

Aya hii inazungumzia hali na mazingira magumu yaliyowakabili Waislamu mwanzoni mwa Uislamu na kueleza kwamba, mbinyo na mashinikizo ya maadui yalikuwa na yalifikia kiwango ambacho waumini waliomba idhini kwa Bwana Mtume SAW awaruhusu wapigane vita na kukabiliana na maadui; wakawa wanasema: kwa nini haziteremshwi aya za kuwapa ruhusa ya kupigana vita? Lakini zilipoteremshwa baadhi ya sura na kutolewa amri ya kujibu uadui wa makafiri, baadhi ya Waislamu waliokuwa wakidai kwa ndimi zao kwamba wako tayari kwa jihadi na mapambano, walirudi nyuma, kufika hadi ya kukodoa macho yao kwa woga na hofu. Kinyume na waumini wa kweli ambao husimama imara katika njia ya jihadi hata kwa kujitolea mhanga maisha yao na kuwa tayari kufa shahidi na kusabilia roho zao katika njia ya Allah, hofu na mshtuko uliwavaa wanafiki, ambao nyoyo zao zina maradhi, kiasi kwamba hata kabla ya vita kuanza roho zilikaribia kuwatoka kwa kihoro. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, yumkini watu wengi wakadai wako hivi na vile kwa ndimi zao, lakini unapofika wakati wa kutekeleza kivitendo hayo wanayodai katika medani ya jihadi na mapambano, hapo ndipo wanapopambanuka waumini na wanafiki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, japokuwa Uislamu ni dini ya rehma, lakini inapolazimu kukabiliana na madhalimu na waonevu, inatangaza jihadi na mapambano na kuwaamuru Waislamu wawalipizie ubaya maaadui sawa na waliowafanyia wao. Wa aidha aya hii inatutaka tufahamu kwamba, kuihofu jihadi na kukimbia kwenye medani ya mapambano ni alama ya udhaifu wa imani na ni unafiki wa batini wa ndani ya nafsi ya mtu. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 931 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase nyoyo zetu na unafiki, na amali zetu na ria, na ndimi zetu na uongo na macho yetu na khiyana, kwani hakika Yeye ni mwenye kuijua khiyana ya macho na yaliyofichikana ndani ya nyoyo zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/