May 27, 2023 04:55 UTC
  • Sura ya Muhammad, aya ya 33-35 (Darsa ya 935)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 935 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 33 ya sura hiyo ambayo inasema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَلَا تُبْطِلُوا أَعْمَالَكُمْ

Enyi mlio amini! Mt'iini Mwenyezi Mungu, na mt'iini Mtume, wala msiziharibu amali zenu. 

Katika darsa kadhaa zilizopita tulisoma aya zilizowazungumzia wanafiki na makafiri. Aya hii ya 33 inawahutubu waumini ya kwamba: Enyi mlioamini! Jihadharini msije mkawa kama wanafiki, mkaasi maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wao wanafiki wamekuwa wakionyesha kwa ndimi zao kwamba wamesilimu na kujisalimisha kwa maamrisho ya Mwenyezi Mungu, lakini katika matendo, ama wamepinga waziwazi au wamekuwa hawatekelezi wajibu na jukumu lao. Kwa hivyo nyinyi, ambao mnajiitakidi kuwa ni waumini wa kweli mliojisalimisha kikamilifu kwa aliyokuamuruni Mwenyezi Mungu na Mtume wake, inapasa muonyeshe kivitendo kwamba mnamtii kikwelikweli Mola wenu; isiwe ni kutekeleza yale yanayoendana na matashi na matakwa yenu na kuyaacha yale yasiyokupendezeni. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, sharti la imani ya kweli ni kujisalimisha na kutii maamrisho ya Allah SWT na Mtume SAW, kwa sababu imani isiyoambatana na kuzitekeleza kivitendo amri za Mwenyezi Mungu na Mtume wake si imani ya kweli. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, mbali na Qur'ani, sira na Sunna za Mtume wa Allah, nazo pia ni hoja ya kisharia. Kwa hivyo ili kuweza kuijua dini vile hasa itakiwavyo, inapasa Muislamu ayazingatie yote hayo mawili. Wa aidha tunajifunza kutokana na aya hii kwamba, kufanya mambo mema na ya kheri peke yake hakutoshi; kuna ulazima pia wa kuzikinga na kuziepusha amali hizo na mambo yanayoziporomosha, kama shirki, ria, ghururi na mtu kuridhishwa na mema yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 34 ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّهِ ثُمَّ مَاتُوا وَهُمْ كُفَّارٌ فَلَن يَغْفِرَ اللَّهُ لَهُمْ

Hakika walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, kisha wakafa na hali ni makafiri, Mwenyezi Mungu hatawaghufiria.

Kwa mujibu wa aya za Qur'ani, Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla ni msamehevu na anaghufiria na kusamehe madhambi mengi sana ya wanaomuasi. Lakini pamoja na hayo, baadhi ya watu hushikilia kubaki kwenye shirki na ukafiri na hata kuwa sababu ya watu wengine pia kupotoka na kutumbukia kwenye lindi la madhambi. Na kwa sababu hiyo, watu hao huishia kuselelea kwenye mwenendo wao huo wa batili hadi mwisho wa uhai wao. Watu kama hao hawajibakishii tena fursa yoyote ya kupata rehma za Mwenyezi Mungu wala kuwa miongoni mwa wanaoghufiriwa na kusamehewa madhambi yao. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu ameuweka wazi mlango wa toba kwa waja wake wote. Lakini watu wanaoamua kuing'ang'ania shirki na ukafiri na kuipinga njia yake Mola, na wakaondoka hapa duniani wakiwa katika hali hiyo, hao hawatapata rehma na msamaha wake. Aya hii inatutaka tujue pia kwamba, nukta muhimu sana kuhusu hatima na mwisho wa maisha ya mtu ni pale anapofikwa na mauti kwa kuondoka duniani akiwa muumini au kafiri. Vilevile aya hii inatuelimisha kuwa, ukafiri unaotokana na kuifanyia haki inadi na ukaidi wa makusudi ni hatari, kwani unamkosesha mtu rehma za Allah SWT.

Tunaihitimisha darsa yetu ya leo kwa aya ya 35 ambayo inasema:

‏ فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّهُ مَعَكُمْ وَلَن يَتِرَكُمْ أَعْمَالَكُمْ

Basi msiregee na kutaka suluhu, maana nyinyi ndio mtakao shinda. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi, wala hatakunyimeni (thawabu) za amali zenu.

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya iliyotangulia na kuwahutubu tena waumini ya kwamba, jihadharini kauli za watu wenye imani dhaifu zisije zikakuathirini, ikawa badala ya kuwa na istikama na kusimama imara mbele ya maadui, mkaamua kupatana na kusikilizana nao. Suluhu na mapatano yanakubalika pale tu adui anapoacha uadui wake na akawa tayari kutambua na kuheshimu haki zenu na kuishi na nyinyi kwa salama na amani. Lakini kufanya suluhu na mapatano na adui, ambaye kila siku yumo mbioni kupanga na kutekeleza njama dhidi yenu, akiwa na dhamira ya kuiangamiza dini ya Mwenyezi Mungu, hiyo ni ishara ya kuwa na imani dhaifu ya dini na kutaka kuwa na raha na wepesi katika maisha ya dunia.  Mwenyezi Mungu anataka waumini wawe na utukufu na sharafu; hivyo kama waumini watakuwa na istikama na msimamo thabiti, Yeye Mola atawawezesha kuwashinda maadui. Lakini wale ambao, kwa sababu ya woga au ulegevu na kupenda kwao raha na wepesi, wanaamua kufanya mapatano na maadui waliowakamia Waislamu na Uislamu, hatua yao hiyo haitakuwa na tija nyingine yoyote kwao isipokuwa kudunika na kudhalilika. Na ni wazi pia kwamba kusimama imara na kukabiliana na adui kwa namna yoyote ile kuna gharama yake; lakini tajiriba na uzoefu umeonyesha kuwa, baada ya muda kupita hubainika kwamba gharama za kufanya mapatano na adui ni kubwa zaidi kuliko za kusimama imara na kukabiliana naye. Isitoshe pia ni kwamba mtu yeyote anayepigania heshima, izza na sharafu ya waumini hata kama atafikwa na machungu na madhara katika njia hiyo, Allah SWT atampa malipo mema na bora na hatampunguzia chochote katika thawabu za amali hiyo ya kheri. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, walioamini, wasiingiwe na woga wala shaka kwa sababu ya uchache wao kwa idadi ya watu na suhula walizonazo, wala kwa wingi wa maadui na suhula walizojizatiti kwazo; kwa sababu Allah SWT yu pamoja na waliomwamini; na yeyote yule ambaye Allah yu pamoja naye mwishowe huwa ndiye mshindi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, imani ya kweli haiendani na ulegevu, ugoigoi na kupenda raha na wepesi. Halikadhalika aya hii inatutaka tujue kwamba, katika medani ya kupambana na adui, waumini hawatangulii kupendekeza suluhu na mapatano, kwa sababu, hiyo ni dalili ya woga, ulegevu na udhaifu, ambalo bila shaka si jambo linalopendeza. Lakini kama yeye adui  ataomba kufanya suluhu na kukawepo na maslaha na manufaa kwa kufanya hivyo, hapo suluhu itakubalika. Na aidha aya hii inatutaka tufahamu kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawatakia waumini izza, heshima na sharafu; na kwa mwongozo wake, anawapa msaada na ushindi watu wanaosimama imara katika njia ya dini yake. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 935 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atulinde na shari za maadui zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/