Jumapili, tarehe 28 Mei, 2023
Leo ni Jumapili tarehe 8 Dhulqaada 1444 Hijria inayosadifiana na tarehe 28 Mei, 2023.
Siku kama ya leo miaka 1096 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Ibn Zubair, mwandishi mashuhuri wa Kiislamu wa wakati huo. Katika ujana wake Ibn Zubair alisoma kwa baba yake elimu muhimu tofauti za wakati huo. Baada ya baba yake kufariki dunia aliutumia utajiri wa baba yake huyo katika njia ya kutafuta elimu, kuasisi maktaba na kuwasaidia wanafunzi wa kidini waliokuwa na hali ngumu ya kimaisha. Mbali na uhodari mkubwa katika uandishi, Ibn Zubair alikuwa na kipawa pia cha kuandika upya baadhi ya vitabu vya wasomi wengine na kuvieneza.

Siku kama ya leo miaka 1065 iliyopita, alifariki dunia Abu Hamid Swaghani, mtaalamu wa nujumu na hesabati wa Iran. Abu Hamid alizaliwa mjini Khurasan, kaskazini mashariki mwa Iran, na baadaye kuhamia mjini Baghdad Iraq. Msomi huyo alihesabika kuwa mmoja wa wasomi wakubwa katika uga wa elimu ya nujumu na hisabati wa zama zake sanjari na kuasisi kituo cha unajimu mjini Baghdad. Msomi huyo ameacha vitabu vingi katika fani ya nujumu.

Siku kama ya leo miaka 1059 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Ali bin Omar Dar-Qutni, mwandishi na mtaalamu wa sheria za Kiislamu. Dar-Qutni alifanya safari nchini Misri na Sham na kuweza kusoma kwa wasomi wakubwa wa zama hizo. Aidha msomi huyo alikuwa hodari pia katika tafsiri ya Qur’an Tukufu, fiq’hi, mashairi na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Miongoni mwa athari zake ni pamoja na vitabu vya ‘as-Sunan’, ‘Sunan Daru Qutni’ na ‘al-Mukhtalif wal-Mu’talif.’

Siku kama ya leo miaka 171 iliyopita, alifariki dunia Eugène Burnouf, mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati wa Ufaransa. Burnouf alizaliwa Paris mwaka 1801 na kuhitimu somo la sheria. Hata hivyo hamu yake kubwa ya kusomea lugha na fasihi sambamba na kuvutiwa na masuala ya Mashariki ya Kati, vilimfanya ajifunze lugha za Sanskrit na Iran ya kale. Eugène Burnouf pia alijifunza utamaduni wa nchi za Iran na India. Miongoni mwa kazi zilizozifanya msomi huyo ni pamoja na kufasiri sehemu za kitabu cha Avesta. Vitabu vya ‘Dondoo za Yasna’ ‘Historia ya dini ya Mabudha’ na ‘Babr Bayan’ ni miongoni mwa vitabu vya Eugène Burnouf. *

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1940, Ubelgiji ambayo ilitangaza kutoegemea upande wowote mwanzoni mwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ilitekwa na majeshi ya Kinazi ya Ujerumani. Majeshi ya Ubelgiji ambayo yalikuwa yakipata usaidizi wa Uingereza, yalisimamisha vita kutokana na amri ya Mfalme Leopold wa Tatu, licha ya kusimama kidete kwa muda wa siku 18 dhidi ya majeshi ya Kinazi ya Ujerumani. Hatua hiyo ya Mfalme Leopold, iliwakasirisha mno wananchi wa Ubelgiji na kuandaa mazingira ya kuondolewa kwake madarakani hapo mwaka 1951.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, sawa na tarehe 28 Mei 1964, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu iliafikiana na fikra ya kubuniwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO ambapo mwanzoni ilizijumuisha harakati nane za mapambano pamoja na idadi kubwa ya taasisi za kielimu, kijamii, kitiba, kiutamaduni na kifedha. Mwaka mmoja baadaye tawi la kijeshi la Fat'h ambalo lilikuwa na wanachama 10,000 likaanzisha shughuli za kupigania ukombozi wa Palestina. Mwaka 1974 PLO ilikubaliwa kuwa manachama mtazamaji katika Umoja wa Mataifa ambapo kufikia mwaka 1982 ilikuwa imeanzisha uhusiano rasmi na zaidi ya nchi 100 za dunia. Taratibu PLO ilianza kupoteza muelekeo wake wa kupambana kijeshi na utawala ghasibu wa Israel ambapo kufikia mwaka 1993, ikiongozwa na Yassir Arafat, ilikubali kuutambua rasmi utawala huo kwa kutia saini mapatano ya Oslo hapo mwaka 1993.

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, yaani tarehe saba Khordad mwaka 1359 Hijria Shamsia duru ya kwanza ya Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (bunge) ilianza. Kufunguliwa duru hiyo ya Majlisi ya kutunga sheria ilikuwa hatua muhimu katika historia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jukumu la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ni kutunga sheria na kusimamia kwa njia ya moja kwa moja utendaji kazi wa rais wa nchi na baraza lake la mawaziri. Hivi sasa Majlisi ina wajumbe 290 ambao huchaguliwa moja kwa moja na wananchi. Kila eneo hupata mbunge kwa kutegemea idadi ya watu wa eneo hilo. Idadi ya wafuasi wa dini za wachache hapa nchini, ingawa haiwezi kufikia kiwango kinachohitajika kwa ajili ya kutengewa mbunge, lakini katiba ya nchi inawapa fursa ya kuwachagua wawakilishi wao bungeni. Vikao vya wazi vya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu hutangazwa moja kwa moja kwa njia ya redio na vile vile magazeti ya nchini hutoa ripoti kuhusu vikao hivyo.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita sawa na tarehe 28 Mei 1991, utawala wa kikomunisti wa Mengistu Haile Mariam ulisambaratika nchini Ethiopia na kupelekea mtawala huyo dikteta kukimbia nchi. Ethiopia ni moja ya nchi kongwe zaidi barani Afrika na wakati mmoja ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Misri ya kale. Tokea karne ya 16 Milaadia wakoloni wa Ureno, Uingereza na Italia walifanya juhudi kubwa za kuikoloni nchi hiyo kwa lengo la kupora utajiri wake lakini bila mafanikio makubwa. Italia iliishambulia Ethiopia mara mbili, shambulio la kwanza likifanyika mwaka 1896 ambapo ilishindwa kufikia malengo yake na la pili likafanyika mwaka 1936 ambapo iliikalia Ethiopia kwa muda wa miaka mitano. Mfalme wa mwisho kuitawala Ethiopia alikuwa Haile Selassie ambaye aliitawala nchi hiyo tokea mwaka 1930 hadi 1974 na kisha akapinduliwa na watawala wa kikomunisti, ambao nao baadaye walikabiliwa na upinzani mkubwa wa ndani kutokana na majanga ya njaa na matatizo mengine yaliyotokana na utawala mbaya.

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 28 Mei 1998, kwa mara ya kwanza Pakistan ilifanya majaribio matano ya makombora ya nyuklia. Majaribio hayo yalifanyika zikiwa zimepita wiki mbili tu tangu hasimu wake, yaani India, ifanye majaribio ya kombora la nyuklia. Baada ya hapo nchi hizo mbili zimekuwa zikifanya kwa zamu majaribio yao ya makombora ya nyuklia. Majaribio ya nyuklia ya Pakistan, kinyume na yale yanayofanywa na India, yamekuwa yakizikasirisha mno nchi za Magharibi za Marekani na Ulaya, na kufikia hatua ya kuiwekea nchi hiyo vikwazo vya kiuchumi.
