Oscar, Hollywood na ubaguzi wa rangi
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kuwa nasi katika Makala ya Wiki. Kipindi chetu leo kitatupia jicho ubaguzi unaofanyika nchini Marekani hususan katika sekta ya filamu ya Hollywood.
Takwimu za hivi karibuni zinazohusiana na suala la mlingano wa mbari na kaumu tofauti katika sekta ya filamu ya Hollywood zinaonesha kuwa, asilimia 12 tu ya flamu na filamu za mfululizo za televisheni ndiyo inayoonesha mlingano halisi wa kaumu za waliowachache katika jamii ya Marekani. Hii inaonesha kuwa, jitihada zilizofanyika kwa miaka kadhaa katika uwanja huo hazikuzaa matunda.
Mwaka 1942 mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Walter White kutoka New York alikwenda Holywood. White alizaliwa Antalanta na wazazi wake walikuwa watumwa. Mababu zao wengi walikuwa wazungu wenye rangi nyeupe. Katika kitabu cha wasifu wake, White anasisitiza sana juu ya suala hilo na kuandika kuwa: Mimi ni Mtu mweusi. Ngozi yangu ni nyeupe, macho yangu ni bluu na nywele zangu zina rangi ya shaba. Vigezo vya mbari yangu havionekani katika dhahiri yangu lakini kwa hali yoyote ile ninajitambua kuwa ninatokana na kizazi cha watu weusi”.
Walter White alikuwa mkuu wa taasisi kubwa zaidi ya kutetea haki za raia nchini Marekani ya National Association for the Advancement of Colored People (NAACP). Wanachama wa jumuiya hiyo wanaamini kwamba, taswira hasi inayooneshwa kuhusu watu weusi nchini Marekani inazidisha chuki na mivutano ya kikaumu nchini humo. White alitaka kuishawishi sekta ya filamu ya Marekani ili itengeneze filamu zinazoonesha taswira chanya na nzuri kuhusu watu weusi. Vilevile alitoa wito wa kuwepo watu weusi zaidi katika visa vinavyojumuisha mbali na kaumu tofauti nchini Marekani.
Hata hivyo takwimu na nyaraka za kihistoria zinaonesha kuwa, juhudi za awali za Walter White za kutaka kubadili sura hiyo katika sekta ya filamu ya Marekani hazikuzaa matunda. Alirubuniwa na vishawishi na taa za Holywood na kupata burudani ya kuzungumza na wacheza filamu na watu maarufu. Ujumbe wake haukuvuka kiwango hicho na kuweza kwenda juu zaidi ya kukutana na kukusanyika kwenye hafla na watu muhimu na alitosheka kwa kutoa taarifa katika vyombo vya habari na kuandika barua tu.
Japokuwa tangu wakati huo kumetokea mabadiliko mengi katika masuala yanayohusiana na kaumu na mbali tofauti nchini Marekani lakini hadi sasa idadi ya watu weusi wanaopewa nafasi za kwanza katika filamu au wanaoalikwa katika zulia jekundu katika mahfali rasmi zinazohusiana na sekta hiyo ya filamu, ni ndogo sana. Ni miaka miwili sasa ambao mtu yeyote mweusi hajawahi kupewa tuzo ya Oscar au hata kuteuliwa kugombea tuzo hiyo katika tukio kubwa zaidi la filamu nchini Marekani.
Takwimu zinaonesha kuwa, watu weusi wametunukiwa tuzo chache sana za Oscar. Watu wenye asili ya Afrika daima wamekuwa wakipewa nafasi za kukariri kariri au za watu mashuhuri katika jamii na ni mara chache sana kuona wakipewa nafasi kuu na asili katika filamu za Holywood. Wacheza filamu wa jamii za waliowachache na weusi wa Marekani daima wamekuwa wakipangiwa kucheza katika nafasi ya mkamilishaji wa mshindi wa filamu na nafasi asili katika filamu hizo wanapewa wazungu na watu wenye ngozi nyeupe.
Sherehe ya Oscar mwaka huu imeambatana na visa na mikasa mingi ambayo imegubika tukio hilo kubwa la filamu za Hollywood na kuathiri fikra za watu wengi. Miongoni mwa mikasa hiyo ni hatua ya wadau wengi wa filamu wa Marekani na hata jumuiya za kutetea haki za binadamu ya kususia sherehe hiyo na kuwasilisha malalamiko kwa watayarishi wake. Mtengeneza filamu mashuhuri wa Marekani, Michael Moore ameunga mkono harakati ya kususia tuzo na sherehe ya Oscar kutokana na kupuuzwa watu weusi katika suala hilo. Mtengenezaji huyo wa filamu za matukio halisi anasema: “Ni maskhara matupu kwamba katika kipindi cha miaka miwili mfululizo hakukua na mchezaji filamu mweusi hata mmoja kati ya arubaini waliochaguliwa kugombea tuzo ya Oscar. Nina matumaini kuwa, hatua hii ya kususia sherehe ya Oscar itakuwa nembo ya kulalamikia suala la kupuuzwa watu weusi”, mwisho wa kunukuu.
George Clooney, mchezaji na mtayarishaji maarufu wa filamu wa Marekani ametoa taarifa akitangaza kuwa Wamarekani wenye asili ya Afrika wana haki ya kusema kuwa, sekta ya filamu ya nchi hiyo haiwawakilishi. Taarifa ya Clooney ambayo imechapishwa katika tahariri ya jarida la Variety inakosoa Academia ya Oscar. Ameandika kuwa: “Tunapaswa kuwa bora zaidi”.
Julie Delpy ambaye ameteuliwa mara mbili kuwania tuzo ya Oscar amesema kuwa wakati mwingine anatamani kuwa Mmarekani mweusi. Delpy ambaye ni mtayarishaji na mchezaji wa filamu anasema: “Miaka miwili iliyopita niliandika makala kuhusu hali hii na kusema kuwa Academia ya Oscar imekuwa taasisi ya ngozi nyeupe na ya kiume, na huu ndio ukweli wa mambo. Wakati huo vyombo vya habari vilinishambulia na kuniraruararua”. <<<>>>>>
Mbali na shakhsia hao mashuhuri wa filamu za Hollywood, wachezaji wengine maarufu kama Will Smith na Dustin Hoffman pia wamelaani hatua ya academia hiyo ya kuwapuuza watu weusi katika tuzo ya Oscar. Hoffman amelalamikia vikali ubaguzi wa rangi uliokita mizizi katika utamaduni wa Marekani na kusema: Katika nchi yetu hii kuna ubaguzi wa rangi ambao haukubadilika hata baada ya kukomeshwa vita vya ndani.
Mcheza filamu huyo mashuhuri anaendelea kusema kuwa: “Sambamba na suala hilo la kutoteuliwa mtu mweusi kugombea tuzo ya Oscar, kuna tatizo kubwa zaidi ambalo ni la polisi kuwaua vijana weusi mitaani. Hili kwa mtazamo wangu ni tatizo kubwa zaidi”, mwisho wa kunukuu.
Mcheza filamu Will Smith amekiambia kipindi cha televisheni moja ya Marekani kwamba: “Mimi ninadhani kuwa tunapaswa kupigana vita ili kuweza kulinda fikra zilizounda nchi yetu na kuipa fahari jamii. Lakini tunapoangalia orodha ya watu walioteuliwa kugombea tuzo ya Oscar hatuoni picha au taswira ya jamii hii”, mwisho wa kunukuu.
Matt Damon mcheza filamu mashuhuri na mzungu wa Marekani huko Hollywood amekosoa sherehe ya Oscar ya mwaka huu. Matt Damon ambaye yeye mwenyewe alikuwa miongoni mwa walioteluliwa kwa ajili ya kuwania tuzo hiyo amesema mara hii hawezi kuketi na kunyamaza kimya. Amesema kuna njia ndefu hadi kufikia utatuzi wa sera za Oscar. “Holywood inapaswa kufanya kazi kubwa zaidi lakini tunapaswa kutambua kwamba dhulma za kijinsia na kimbari zilizopo nchini Marekani ni kubwa zaidi ya kuweza kuzihusisha tu wateule wazungu wa tuzo ya mwaka huu ya Oscar. Tatizo hilo limekita mizizi katika sekta ya biashara ya Hollywood au kwa kwa maneno sahihi zaidi, katika nchi nzima ya Marekani”, amesisitiza Matt Damon.
Spike Lee ambaye ni mkurugenzi, mtayarishaji na mwandishi filamu mweusi wa Marekani amewatuhumu viongozi wa Hollywood kuwa hawawapi Wamarekani weusi nafasi nzuri zinazopelekea kutunukiwa tuzo ya Oscar. Lee anasema miongoni mwa sababu za jambo hilo ni uchache wa viongozi weusi katika sekta ya filamu ya Marekani. Spike Lee anasema ni rahisi kwa Mmarekani mweusi kuwa rais wa Marekani kuliko kuwa mkuu wa studio ya kutengeneza filamu.
Chris Rock ambaye alikuwa mwendeshaji wa sherehe ya mwaka huu ya Oscar pia alionesha msimamo mkali wa kupinga ubaguzi katika sekta ya filamu ya Marekani mwanzoni mwa kutolewa tuzo hiyo. Mchezaji huyo wa filamu za kuchekecha (Comedy) ameashiria mkasa uliotokea kwenye sherehe ya Osar mwaka huu na kupuuzwa Wamarekani weusi katika kuteuwa wagombea wa tuzo hiyo na kuhoji: “Je, Holywood imekuwa na ubaguzi wa rangi? Ninyi watu wa Holywood ni wabaguzi wakubwa wa rangi”.
Chris Rock amewaambia hadhirina kwamba: “Sisi Wamarekani weusi tunataka kupewa fursa. Wacheza filamu weusi wanataka fursa sawa na wenzao wazungu”.
Alaa kulli hal, sherehe ya Oscar ya mwaka huu imeambatana na makelele na malalamiko mengi ya kubaguliwa wacheza filamu weusi licha ya propaganda kubwa zilizofanyika kabla na wakati wa tukio hilo kubwa la filamu la Hollywood.