May 19, 2021 11:25 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran akosoa kimya cha jamii ya kimataifa kwa jinai za Israel

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa , asasi za kibinadamu na Umoja wa Mataifa kwa jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.

Muhammad Baqir Qalibaf amesema hayo leo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Marzouq Ali al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo yake na maspika wa mataifa ya Kiislamu kuhusiana na hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Israel huko katika Ukanda wea Gaza.

Katika mazungumzo yake hayo, Spika wa Bunge la Iran ameashiria unyama na jinai za Israel zisizo na kikomo zinazofanyika kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani na kueleza kwamba, hii leo maumivu ya pamoja ya mataifa ya Kiislamu ni kumwagwa damu za wanawake na watoto wadogo wa Kipalestina.

Spika Qalibaf amesema, mazingira yaliyoko hivi sasa katika ardhi za Waislamu ni ya maafa na uchungu zaidi kutokkana na jinai dhidi ya binadamu zinazofanyika.

Hujuma na mashambulio ya Israel dhidi ya ukanda wa Gaza

 

Amesema, licha ya jinai zote hizo lakini inashangaza kuona kwamba, jamii ya kimataifa, asasi za masuala ya kibinadamu na Umoja wa Mataifa zimenyamaza kimya.

Kwa upande wake, Marzouq Ali al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait amesema kuwa, matukio ya Gaza na Palestina ni jinai dhidi ya Waislamu wa eneo hili.

Amesisitiza kuwa, kulindwa umoja na mshikamano wa mataifa yote ya Kiislamu mkabala na dhulma, ukandamizaji na upendaji makuu wa Wazayuni ni wajibu wa kisheria, kibinadamu, Kiislamu na kimaadili.

Tags