Aug 02, 2021 05:54 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Agosti 2

Hujambo ashiki na mfuatiliaji wa masuala ya spoti natumai huna neno. Karibu tutupie jicho baadhi ya matukio makubwa na muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbalimbali za dunia.

Soka; Persepolis watwaa ubingwa wa IPL

Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini baada ya kuichachafya klabu ya Paykan katika mchuano wa aina yake siku ya Ijumaa. Katika kipute hicho cha kukata na shoka, vijana wa Persepolis au ukipenda waite Wekundu wa Tehran waliwabamiza Watengeneza Magari wa Iran mabao 2-0 katika mchezo huo uliopigwa katika Uwanja wa Shahr-e Qods jijini Tehran, na hiyo kutwaa taji hilo kwa mara ya tano mfululizo. The Reds walianza kwa kasi nzuri na kutawala mchezo huo wa fainali ya duru ya 20 ya IPL, huku kiungo Mehdi Abdi akifunga bao la kwanza baada kupokea pasi safi ya chini kwa chini kutoka kwa somo yake Mehdi Torabi, kunako dakika ya 8 ya mchezo. Ahmad Nourollahi alifanya mambo kuwa 2-0 kwa bao lake la dakika ya 21.

Persepolis, mabingwa IPL msimu huu

Persepolis ambayo ilishinda taji hili kwa mara ya kwanza katika msimu wa ligi ya mwaka 2001-2002 huku wakitwaa ubingwa huo mara ya pili katika msimu wa mwaka 2007 na 2008, wameshinda msimu huu kwa alama 67, alama mbili zaidi ya Sepahan. Klabu ya Sepahan ambayo ilitwaa Ligi Kuu ya Soka ya Iran katika misimu ya mwaka 2002-03, 2009-10, 2010-11, 2011-12 and 2014-15, imemaliza katika nafasi ya pili msimu huu, mbele ya Esteqlal inayokamilisha orodha ya tatu bora kwa alama 56. Sepahan iliibamiza The Blues ya Tehran mabao 2-1 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliochezwa katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran.

Iran bingwa wa Futsal Asia

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa mashindano ya mchezo wa soka aina ya futsal inayopigwa ukumbini ya Asia, baada ya kuibamiza Thailand katika fainali iliyochezwa Ijumaa. Katika mchezo huo wa kukata na shoka, Team Melli ya Iran kama inavyofahamika hapa nchini iliinyoa bila maji Thailand, kwa kuigaragaza mabao 5-1. Mabao ya timu hiyo ya taifa ya kandanda ya ukumbini ya Iran yalifungwa na Alireza Rafieipour (2), Behzad Azimi (2) na Farhad Tavakoli aliyepachika kambani bao moja.

Timu ya futsal ya Iran

Mapema siku hiyo ya Ijumaa, Uzbekistan iliitibua Misri mabao 4-0 na kuibuka mshindi wa tatu. Mashindano hayo ya kibara yalifanyika jijini Bangkok nchini Thailand kati ya Julai 25 na 30. Iran ambao ni mabingwa nambari moja wa mchezo wa futsal barani Asia inajiandaa kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwenye mchezo huo mwaka huu 2021, zitakazotifua mavumbi huko Lithuania kuanzia Septemba 12 hadi Oktoba 3. Timu hiyo ya Iran imepangwa katika Kundi F pamoja na mabingwa watetezi Argentina, Marekani na Serbia.

Soka Cecafa; Tanzania bingwa U-23

Tanzania ndiyo mabingwa wa Kombe la CECAFA kwa vijana wenye umri chini ya miaka 23 msimu huu. Hii ni baada ya kuichachafya Burundi mabao 6-5 kupitia mikwaju ya penati, katika mchuano wa fainali wa taji hilo la Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA uliopigwa nchini Ethiopia.

Cecafa

Timu hiyo ya mabarobaro wa Tanzania ilitinga fanali baada ya kuipepeta Sudan Sudan Kusini bao moja bila jibu katika mchuano wa nusufainali, wakati ambapo Burundi ilikuwa inajikatia tiketi ya fainali hiyo kwa kuigaragaza Kenya mabao 4-2 kupitia mikwaju ya penati.

Kombe la Kagame

Mechi ya ufunguzi ya mashindano ya Kombe la Kagame 2021 kati ya Yanga ya Tanzania na Nyasa Big Bullets ya Malawi imemalizika kwa sare ya bao 1-1. Chini ya Kocha Mkuu, Razak Siwa, Yanga ambayo iliwaarifisha wachezaji wake wapya kwenye mchuano huo, ilikuwa ya kwanza kucheka na nyavu katika mechi hiyo ya ufunguzi. Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa sare ya bao 1-1, mabao yaliyofungwa na Waziri Junior kwa upande wa Yanga akifunga dakika ya 7, kabla ya Chiukepo Msowoya kuisawazishia Nyasa dakika ya 29 kwa mkwaju wa penati baada ya Abdalah Shaibu ‘Ninja’ wa Yanga kumpiga kiatu Babatunde Adepoju wa Nyasa. Kipindi cha pili kilirejea kwa timu zote mbili kuanza kwa kasi kila moja ikitafuta bao la kuongoza lakini hadi kipengya cha kumaliza ngoma kinapigwa, hakuna aliyekuwa amefanikiwa kupata bao jingine.

Dondoo za Olimpiki

Mwanajudo wa Lebanon, Abdullah Miniato ametangaza kujiondoa katika mashindano ya kimataifa ya mchezo wa mixed martial arts (MMA) huko mjini Sophia, Bulgaria, na kwa utaratibu huo anakuwa judoka wa tatu kukwepa kuvaana na hasimu kutoka utawala haramu wa Israel katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020. Judoka huyo pamoja na mkufunzi wake Muhammad Al-Gharbi, wametangaza kujiondoa kwenye mpambano huo wa kimataifa, baada ya droo iiyochezeshwa jana Jumamosi kumpanga barobaro huyo achuane na hasimu Mzayuni. Hatua hii ni mwendelezo wa upinzani dhidi ya utawala haramu wa Israel ambao umeendelea kupata pigo katika mashindano yanayoendelea ya Olimpiki ya Tokyo 2020 nchini Japan. Hii ni baada ya wanajudo wengine wawili kutoka Algeria na Sudan kukataa kupambana na washindani wao kutoka Israel.

Mwanajudo wa Lebanon, Abdullah Miniato

 

Majudoka hao ni Mohamed Abdalrasool wa Sudan na Fat'hi Nourin wa Algeria. Fath-i Nurin, ambaye kwa sababu ya kutokubali kuutambua utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na kwa ajili kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina hakuwa tayari kupambana na mshindani kutoka utawala huo katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo 2020, amesema, amefurahia hatua yake hiyo kwa kuwa imeikasirisha Tel Aviv. Ameongezea kusema: "uamuzi niliochukua, kwanza ni wa kujivunia mimi mwenyewe na kisha ni hatua ya fahari na kujivunia kwa wananchi na serikali ya Algeria, kwa sababu Rais wa nchi yetu Abdelmadjid Tebboune naye pia ameitangazia dunia nzima kwamba, sisi hatuoni kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kuwa ni tukio la kheri na tunaunga mkono malengo matukufu ya watu wa Palestina." Fat-hi Nurin amesisitiza kwa kusema: "Nimefurahi kuona utawala wa Kizayuni umekasirika na kutokana na kutumiwa jumbe za kuungwa mkono katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu." Gazeti la Kiebrania la Yediot Ahronot liliandika katika toleo lake la hivi karibuni kuwa, historia imethibitisha kuwa ukweli hauwezi kubadilishwa na kwamba mapatano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu yako makaratasini tu, lakini katika mazingira halisi ya mahusiano ya kiutu, wanamichezo wa nchi za Kiarabu wamethibitisha kuwa, kwa mtazamo wao, hakuna nchi inayoitwa Israel.

Aprili mwaka jana, Shirikisho la Judo Duniani (IJF) lililipiga marufuku ya miaka minne Shirikisho la Judo la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIJF) baada ya Tehran kulitaka lisiwapange wanamichezo wake mkabala na mahasimu wa Israel.

Huku hayo yakijiri, IJF imeipongeza Saudi Arabia baada ya mwanamichezo wa kike wa nchi hiyo ya Kiarabu kukubali kupambana na Mzayuni katika mashindano ya Olimpiki ya Tokyo.

Dondoo za Hapa na Pale

Wachezaji wasiopungua watano wa soka wameuawa katika mlipuko wa bomu kwenye basi lililokuwa limebeba timu ya mpira wa miguu katika mji wa Kismayo huko kusini mwa Somalia. Afisa mmoja wa polisi ya Somalia amesema bomu lililokuwa limetegwa kwenye basi la timu ya mpira wa miguu ya JCCI lililipuka muda mfupi baada ya basi kung'oa nanga likielea uwanjani kwa ajili ya mechi ya ufunguzi wa mashindano ya kanda ya Jubaland. Kapteni Ahmed Farah amesema kuwa, wachezaji 5 wamethibitika kuuawa na wengine zaidi ya 12 wamejeruhiwa. Rais Mohamed Abdullahi Farmaajo wa Somalia ametuma salamu za rambirambi kwa familia za wahanga wa shambulizi hilo na kulituhumu kundi la al Shabab lenye mfungamano la al Qaida kuwa ndilo lililohusika na hujuma hiyo.

Maafisa usalama wakikagua eneo la mripuko Mogadishu

Mbali na hayo, waendesha baiskeli 42 wameanza mbio za kuhamasisha ushirikiano ndani ya Afrika Mashariki katika duru ya nne ya mashindano ya Great African Cycling Safari’ na wanatarajiwa kupita katika majiji sita kabla ya kuhitimisha mashindano hayo. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk amezindua mashindano hayo Jijini Dar es Salaam na kusema ni muhimu kwa jumuia. Washiriki hao wataendesha baiskeli kwa zaidi ya kilomita 6000 kwa kupita katika Miji Mikuu ya Mataifa hayo ikiwemo, Dodoma (Tanzania), Nairobi (Kenya), Kampala (Uganda), Kigali (Rwanda) na Bujumbura (Burundi). Mashindano hayo yatahitimishwa Jijini Arusha.

Balozi Mbarouk anasema, “Hii ni alama kubwa ya ushirikiano kwa nchi za Afrika Mashariki na zaidi yanahimarisha ushirikiano wetu, sisi kama viongozi wa Jumuiya tunaona kwa namna gani ya kuishauri Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuyaweka mashindano haya katika kalenda yake ili pamoja na mambo mengine yawe katika utaratibu unaotambulika.” Naye Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu, amesema mashindano hayo yatasaidia kutangaza vivutio mbalimbali vilivyopo katika nchi za Afrika Mashariki sambamba na kuwavutia watu wengi zaidi kuja na kushiki mashindano hayo. Amesema mashindano ‘Great African Cycling Safari’ yanayohusisha umbali wa Kilomita 6000 yakitumia siku 55, yana mvuto zaidi ya yale yanayojulikana kama ‘Tour de France’ ya nchini Ufaransa.

Na klabu ya Simba ya Tanzania imefikia uamuzi wa kumtema msemaji wa timu hiyo mashuhuri ya soka, Haji Manara. Uongozi wa klabu hiyo umemteua kaimu katibu mkuu wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga kukaimu nafasi hiyo ya Manara. Inaelezwa uhusiano usioridhisha na wanahabari, baadhi ya wadau wa soka na utovu wa nidhamu kwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez ni sababu zilizochangia kwa kiasi kikubwa kumng’oa Manara ndani ya nafasi hiyo iliyompatia umaarufu mkubwa hasa dhidi ya Yanga.

……………………..TAMATI….…….…….

 

 

Tags