UN yalaani mapinduzi ya kijeshi Niger; wananchi waandamana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i100384-un_yalaani_mapinduzi_ya_kijeshi_niger_wananchi_waandamana
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa akilaani vikali mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa Niger.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 27, 2023 07:23 UTC
  • UN yalaani mapinduzi ya kijeshi Niger; wananchi waandamana

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa akilaani vikali mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Mohamed Bazoum wa Niger.

Stephane Dujarric, Msemaji wa Antonio Guterres amesema Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesikitishwa mno na kitendo hicho cha kuondolewa madarakani Rais Bazoum, kinyume na Katiba ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Taarifa hiyo imesema: Guterres ametoa mwito wa kukomeshwa vitendo vyote vinavyohujumu misingi ya demokrasia nchini Niger, na kuzitaka pande zote husika kujiepusha na ghasia na kuheshimu utawala wa sheria.

Guterres ameeleza bayana kwenye taarifa hiyo kuwa, Umoja wa Mataifa unaiunga mkono na unasimama na serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na taifa la Niger kwa ujumla.

Wakati huohuo, watetezi wa demokrasia nchini humo wamefanya maandamano katika mji mkuu Niamey, kumuunga mkono Rais Bazoum aliyepinduliwa.

Huku wakiwa wabeba picha za Rais Bazoum, waandamanaji hao ambao akthari yao walikuwa vijana wamesema watasimama kidete kutetea jamhuri na taasisi za kidemokrasia nchini, huku wakilaani mapinduzi hayo. 

Guterres na Rais Bazoum walipokutana Niamey huko nyuma

Kadhalika viongozi wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) wamelaani mapinduzi hayo ya kijeshi Nigeria na wametaka Rais Bazoum aachiliwe huru bila masharti yoyote na wanajeshi warejee kwenye kambi zao.

Bazoum, ambaye ni mshirika wa karibu wa Ufaransa, alichaguliwa kuwa rais katika uchaguzi wa 2021 ambao ulikuwa wa kwanza wa mpito wa mamlaka ya kidemokrasia katika nchi hiyo ambayo imeshuhudia mapinduzi manne ya kijeshi tangu uhuru kutoka kwa Ufaransa mnamo 1960.

Rais huyo aliyepinduliwa amesema katika ujumbe wa mtandao wa kijamii wa X (Twitter) leo Alkhamisi kuwa, atafanya kila awezalo kulinda mafanikio ya kidemokrasia yaliyopatikana nchini humo. Ametoa mwito kwa wanademokrasia na wazalendo wote kufanya juu chini kuhakikisha kuwa mapinduzi hayo yanafeli.

Wanajeshi wa Niger wakitangaza mapinduzi dhidi ya serikali ya Bazoum

Akisoma taarifa, Kanali Amadou Abdramane, aliyeandamana na maafisa wengine tisa, alisema vikosi vya ulinzi na usalama vya Niger vimeamua kumpindua Bazoum kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbaya.