Kuendelea mgogoro wa Sudan; kujiuzulu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa
Vita nchini Sudan vingali vinaendelea na pande mbili zimeendelea kung'ang'ania misimamo yao hali ambayo imezifanya juhudi za kuhitimisha vita hivyo kutozaa matunda.
Katika hali hii, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, ametangaza kujiuzulu akionya kuwa Sudan inakaribia kuingia kwenye vita visivyodhibitika vya wenyewe kwa wenyewe.
Volker Perthes, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, alisema juzi Jumatano kwamba: "Ni fakhari kwangu kuhudumu kama Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kwa zaidi ya miaka miwili na nusu. Lakini nimemuomba Katibu Mkuu aniondoe katika nafasi hii, hivyo hii itakuwa ni taarifa yangu ya mwisho katika nafasi hii."
Katika taarifa yake ya hivi karibuni Perthes alionya kwamba "hakuna ishara za kupungua vita nchini Sudan, na kile kilichoanza kama mzozo kati ya makundi mawili ya kijeshi kinaweza kugeuka kuwa vita kamili vya wenyewe kwa wenyewe."
Kujiuzulu mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan kunafanyika miezi mitatu tu baada ya serikali ya Khartoum kutangaza kuwa, afisa huyo wa UN ni mtu asiyefaa. Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, mkuu wa serikali ya kijeshi la Sudan, alimtuhumu Perthes kuwa ni mtu mbaguzi ambaye haheshimu "utawala wa taifa" la Sudan kama alivyosema.
Vita nchini Sudan vinaendelea na vimeshika kasi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo na kuwafanya wananchi wa nchi hiyo kukabiliwa na hali mbaya. Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RFS) kinachoongozwa na Hamdan Dagalo kimedai katika taarifa yake ya hivi karibuni kwamba, katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jeshi la Sudan limeua watu 104 na kuwajeruhi mamia ya wengine.
Mzozo na hitilafu baina ya ya Abdul Fattah al-Barhan, Mkuu wa Baraza la Utawala na kamanda wa jeshi la Sudan, na Mohammad Hamdan Dagalo, kamanda wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka, baada ya kusainiwa "mkataba" wa kuunda kipindi cha mpito na kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia, ulijitokeza waziwazi na kufuatia hilo, Aprili 15 mwaka huu kukaanza vita kati ya jeshi na kikosi cha RSF. Hadi sasa, upatanishi wa kimataifa wa kumaliza mzozo huo na hata juhudi za vikao vya pande hasimu katika meza ya mazungumzo hazijazaa matunda.
Mapigano haya mbali na Khartoum na Omdurman yanaendelea pia katika maeneo tofauti ya Sudan. Ripoti zinaonyesha kuwa, mapigano kati ya jeshi na vikosi vya msaada wa haraka vya Sudan yameshadidi pia katika majimbo ya Kordofan Kaskazini na Darfur Kusini. Kuhusiana na suala hilo Umoja wa Mataifa nchini Sudan umetangaza kugunduliwa kwa makaburi 13 ya halaiki katikati ya jimbo la Darfur lililopo kaskazini-magharibi mwa Sudan na katika mpakani mwa Chad. Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan umetangaza kuwa, makaburi hayo ya umati ni natija ya mashambulio ya Kikosi cha Usaidizi wa Haraka na wanamgambo wa kiarabu dhhidi ya raia ambapo akthari yao ni watu wa kabila la Masalit.
Hali ya mambo nchini Sudan ni mbaya. Mashambulizi ya pande zote mbili yameongezeka na uingiliaji wa kigeni unaendelea moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika nchi hiyo, kiasi kwamba, kamanda mkuu wa jeshi la Sudan yumo katika mashauriano na baadhi ya nchi za eneo hilo, kama vile Misri, na kamanda wa vikosi vya msaada wa haraka pia ameanza mazungumzo na baadhi ya nchi nyingine. Kwa upande mwingine, uingiliaji kati wa Marekani unaendelea katika kivuli cha juhudi za kuleta amani katika nchi hiyo.
Kuhusiana na hilo, gazeti la kikanda la "Rai El Youm" hivi karibuni liliandika kuhusu nafasi haribifu ya Marekani nchini Sudan: Sudan ni mhanga wa njama ya Marekani na Israel ya kulipiza kisasi misimamo ya nchi hii katika miaka hivi karibuni ya kuunga mkono Palestina, na kwa msingi huo nchi hii ya Kiafrika imeendelea kutwishwa vita na hadi kufikia sasa juhudi za kieneo na kimataifa za kukomesha vita hivyo zimefel.
Hata kama mashirika ya kimataifa yameonya kuhusu hali mbaya nchini Sudan, lakini kivitendom mzozo unaoendelea umeifanya kuwa muhali hatua yoyote ya kuwafikishia misaada wananchi wa nchi hiyo.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Turk, alitoa wito wa kuweko irada na azma ya kisiasa yenye uratibu wa jamii ya kimataifa kwa kumaliza janga la vita nchini Sudan. Amesema: Sisi tunahitaji kuwa na irada ya kisiasa yenye uratibu na ushirikiano wa watu wenye ushawishi katika jamii ya kimataifa kwa ajili ya kuhitimisha maafa ya kibinadamu nchini Sudan. Hivyo basi kuna haja ya kusitisha vita hivyo kabla ya kuchelewa sana.
Filihali, mwakilishi wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan amejiuzulu huku kivitendo nchi hiyo ikiwa imetumbuikia pakubwa katika vita na endapo hali hii itaendelea, vita vya Sudan vinaweza kuenea katika nchi nyingine za Afrika pia. Inaonekana kuwa katika hali ya sasa, upatanishi na mazungumzo ya vikundi vya kisiasa vya ndani na wahusika kwenye mzozo na kusitishwa kwa uingiliaji wa kigeni kunaweza kwa kiwango fulani kuandaa mazingira ya usitishaji mapigano.
Kuhusiana na hili, Suleiman Sandal, kiongozi wa Vuguvugu la Haki na Usawa la Sudan ametangaza kuwa: Jamhuri ya kwanza (iliyoafikiwa - baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Omar al-Bashir) haikuweza kuongoza serikali na tofauti zimesababisha kuibuka vita huko Khartoum; kwa muktadha huo, kuna haja ya jamhuri ya pili kuanzishwa nchini Sudan ambayo itajumuisha mfumo wa serikali ya kiraia, kidemokrasia, mamlaka ya muundo wa shirikisho juu ya nchi na kuchaguliwa wa rais kwa maafikiano.