Maandamano ya kuwaunga mkono Wapalestina yafanyika tena Afrika Kusini
Kwa mara nyingine, wananchi wa Afrika Kusini wamefanya maandamano wakionyesha mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, mamia ya Waafrika Kusini walitangaza uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina katika maandamano ya jana Ijumaa mjini Cape Town.
Waandamanaji hao wanaopinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watu wa Gaza wamekosoa uamuzi wa serikakli ya Washington wa kutuma silaha zaidi huko Israel kuisaidia serikali ya kifashisti na kibaguzi na Benjamin Netanyahu kuendeleza mauaji ya kutisha dhidi ya raia wasio na hatia wa Gaza.
Waungaji mkono wa Palestina nchini Afrika Kusini pia wametoa wito wa kufukuzwa balozi wa Israel nchini mwao, mbali na kulaani utawala huo kwa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina na kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni.
Maandamano kama hayo yalifanyika mjini Cape Town siku ya Jumatano, ambako washiriki walisisitiza haja ya kukomeshwa ukatili na uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza.
Mandla Mandela, mjukuu wa hayati Nelson Mandela ambaye ni mmoja wa washiriki wa maandamano ya jana Ijumaa mjini Cape Town amesisitizia haja ya kukomeshwa ukatili na uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Amesema, "Namuasa Rais Cyril Ramaphosa asizungumzie tu kadhia ya Palestina katika jukwaa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, bali achukue hatua za kivitendo."
Aidha amemtaka Waziri wa Uchukuzi wa nchi hiyo alifutie leseni shirika la usafiri wa anga la utawala wa Kizayuni wa Israel la El Al.