Sita wauawa baada ya mabasi kufyatuliwa risasi Mandera Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10372-sita_wauawa_baada_ya_mabasi_kufyatuliwa_risasi_mandera_kenya
Watu wasiopungua sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kuyamiminia risasi mabasi mawili hii leo katika kaunti ya Mandera nchini Kenya kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 01, 2016 10:50 UTC
  • Wanamgambo wa ash Shabab wa Somalia
    Wanamgambo wa ash Shabab wa Somalia

Watu wasiopungua sita wameuawa baada ya watu wenye silaha kuyamiminia risasi mabasi mawili hii leo katika kaunti ya Mandera nchini Kenya kwenye mpaka wa nchi hiyo na Somalia.

Fredrick Shisia, Kamishna wa Kaunti ya Mandera amesema kuwa, tukio hilo limetokea leo saa tatu na nusu asubuhi kwa majira ya eneo hilo wakati mabasi mawili hayo yalipokuwa yanaelekea katika mji wa Mandera kutokea jijini Nairobi.

Kamishna Shisia ameongeza kuwa, hadi tunaandika habari hii watu sita wamethibitishwa kuuawa katika ufyatuaji risasi huo. Ripoti zinasema kuwa basi la kwanza lilipigwa risasi na watu wwenye silaha likiwa kati ya miji ya Elwak na Wargadud na basi la pili lijulikano kwa jina la E-Coach lilishindwa kuendelea na safari baada ya kupigwa risasi. Wengi wa waliouliwa walikuwa katika basi la pili. Abiria waliojeruhiwa wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha Afya cha Wargadud. Polisi mmoja wa Kenya ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye shambulio hilo na polisi mwingine mmoja amejeruhiwa. Polisi hao walikuwa wakiyasindikiza mabasi hayo. Polisi ya kaunti ya Mandera jana ilitahadharisha kuhusu safari za mabasi katika eneo hilo hadi utakapomalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani kutokana na vitisho vya usalama vilivyotolewa na wanamgambo wa kundi la al Shabab wenye makao yao makuu nchini Somalia. Tayari polisi imeanzisha oparesheni ya kuwasaka wahusika wa jinai hiyo.