Dec 06, 2023 03:39 UTC
  • Zoezi la uokoaji laendelea Hanang huku Tanzania ikiomba msaada wa kimataifa kwa wahanga wa maporomoko

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiomba jumuiya za kimataifa na taasisi za ndani kusaidia juhudi za serikali ya nchi hiyo za uokoaji na kutafuta maiti wa maporomoko ya tope pamoja na misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa wilaya ya Hanang mkoani Manyara.

Mwito huo umo kwenye taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania huku taarifa nyingine zikisema kuwa, idadi ya waliofariki kutokana na maafa ya mvua zilizosababisha mafuriko na maporomoko ya tope imekaribia watu 70 na zaidi ya watu 116 wamejeruhiwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Jumanne.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika mji wa Katesh, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi, Majaliwa alisema ofisi yake imepewa jukumu la kuratibu misaada ya kibinadamu inayotolewa na mashirika ya ndani na nje ya nchi pamoja na kutoka kwa wafanyabiashara na watu binafsi.

Maporomoko ya tope na udongo yameisababishia hasara kubwa Wilaya ya Hanang, Mkoani Manyara huko Tanzania

 

Juzi Jumatatu, ofisi ya rais wa Tanzania ilisema takriban watu 5,600 wamepoteza makazi yao na zaidi ya hekta 750 za mazao ya shambani zimeharibiwa.

Huku hayo yakiripotiwa, zoezi la kuwaokoa waathirika wa maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang mkoani Manyara iliingia siku ya tatu jana, huku jana asubuhi hali ya hewa ikibadilika na kuanza kunyesha tena.

Aidha wananchi walionekana jana wakiendelea kuokoa vitu mbalimbali katika nyumba zao na wengine katika sehemu za biashara.

Kwa mujibu wa mamlaka za hali ya hewa za serikali ya Tanzania, mvua kubwa zilianza kunyesha majira ya saa 11:00 alfajiri ya Jumapili na zikasababisha mafuriko yaliyoporomosha tope kutoka Mlima Hanang, ambao ni mlima wa Volkano ulio na urefu wa mita 3,418 juu ya usawa wa bahari.

Tags