UN yalaani mauaji ya wakili wa haki za binadamu Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10663-un_yalaani_mauaji_ya_wakili_wa_haki_za_binadamu_kenya
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani vikali mauaji ya wakili wa haki za binadamu nchini Kenya Bwana Willie Kimani, mteja wake Josphat Mwenda, na dereva wao wa taxi Joseph Muiruri, yaliyofanyika Juni 23.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 06, 2016 00:02 UTC
  • UN yalaani mauaji ya wakili wa haki za binadamu Kenya

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imelaani vikali mauaji ya wakili wa haki za binadamu nchini Kenya Bwana Willie Kimani, mteja wake Josphat Mwenda, na dereva wao wa taxi Joseph Muiruri, yaliyofanyika Juni 23.

Watatu hao walitoweka baada ya Bwana Kimani na Bwana Mwenda kuhudhuria kesi hakama ya Mavoko, kilometa 30 Mashariki mwa Nairobi, kesi inayomhusisha afisa katika utawala wa polisi.

Mwenda alipigwa risasi na kuumizwa na polisi Aprili 2015 na kisha kufunguliwa mashtaka ya uongo ya uhalifu.

Willie Kimani, ambaye alikuwa akifanya kazi kwenye shirika lisilo la kiserikali la International Justice Mission, alikuwa akimsaidia Mwenda katika kesi yake. Maiti zao zenye ishara ya kuteswa zilikutwa mtoni Juni 30 Kaskazini Mashariki mwa Nairobi.

Rupert Colville ambaye ni msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ametoa wito kwa serikali ya Kenya kuwachukulia hatua za kisheria wahiska wa jinai hiyo. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa mwanasheria mkuu wa Kenya amemhakikishia kwamba jitihada ziote zitafanyika ili kubaini waliohusika katika mauaji hayo na kwamba Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Kenya ametangaza kuwa uchunguzi wa kina utafanyika.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameitaka serikali ya Kenya kuchukua hatua za kuzuia ongezeko la mauaji ya kiholelea na vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.