Mar 15, 2024 07:41 UTC
  • Mgomo wa nchi nzima wa madaktari Kenya waacha wagonjwa wakitangatanga, utoaji huduma wakwama

Madaktari kote nchini Kenya wamewaacha wagonjwa wakitangatanga baada ya kugoma kuhudumu katika hospitali za umma jana Alkhamisi, licha ya agizo la Mahakama la kuzuia mgomo wa kitaifa wa madaktari hao.

Mgomo huo unaohusishwa na Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno wa Kenya (KMPDU) ambalo ni shirika kubwa zaidi la wataalamu wa tiba nchini Kenya, lenye zaidi ya wanachama 8,000, umesababisha usumbufu mkubwa katika mfumo wa huduma za afya nchini humo na kulemaza utoaji huduma muhimu.
 
Ripoti kutoka Nairobi, Mombasa, Eldoret, Migori, Nyeri, na Kisumu zinatoa taswira ya hali ya fujo na mfadhaiko.
 
Steve Ndonga, afisa wa KMPDU mjini Kisumu amesema, muungano huo hautambui agizo la Mahakama kwa sababu halitumiki kwa hospitali zote.
Hali katika Hospitali ya umma ya Kenyatta

Wagonjwa wanaotafuta huduma ya dharura, uchunguzi wa kawaida na taratibu muhimu walikataliwa kupokelewa na wafanyakazi waliozidiwa na wagonjwa au kulazimishwa kutafuta matibabu mbadala, ambayo mara nyingi ni ghali zaidi katika vituo vya matibabu vya binafsi.

 
Dk. Khalib Salum wa Hospitali Kuu ya Pwani, amevieleza vyombo vya habari: "kwa sasa tunatoa huduma muhimu pekee, hasa za dharura. Huduma zisizo za dharura hazipatikani kwa muda na wodi kadhaa zimefungwa kutokana na uhaba wa wafanyakazi kutokana na mgomo".
 
Daktari huyo ameongezea kwa kusema: "uamuzi wetu wa kupunguza huduma unasukumwa na hitaji la kuboreshwa kwa mazingira ya kazi kuhusu wafanyakazi, kati ya malalamiko mengine mengi".
 
Hali ni ya kusikitisha hasa kwa wagonjwa walio na maradhi sugu ambao wanahitaji huduma ya matibabu ya mara kwa mara. Wengi wamelazimika kukimbilia kliniki za kibinafsi za gharama kubwa.
 
KMPDU inashikilia kuwa mgomo huo ndilo suluhisho la mwisho la kushughulikia malalamiko yao, hasa yanayohusu kucheleweshwa kwa upangaji wa wahudumu wa afya, jambo ambalo limesababisha upungufu wa wafanyakazi, huku kukicheleweshwa kutumwa wahitimu wa matibabu 1,200 katika hospitali.
 
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha amepuuzilia mbali matakwa ya KMPDU na kusema kuwa hayatekelezeki, akitaja kutokuwa na mamlaka wizara ya kutuma wahitimu wa matibabu.
Nakhumicha amesisitizia pia hali halisi ya uhaba uliopo kutokana na ufinyu wa bajeti.../

 

Tags