Wanajeshi 25 wahukumiwa kifo Kongo kwa kumkimbia adui
Jumla ya washtakiwa 31, wakiwemo wanajeshi 27 na wake zao wanne ambao ni raia wa kawaida wamefikishwa katika mahakama ya kijeshi ya Butembo katika mkoa wa Kivu Kaskazini, karibu na mstari wa mbele wa vita kwa "kutoroka vitani na kumpa nafasi adui".
Jules Muvweko wakili upande wa utetezi ameeleza kuwa wateja wao wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo kumkimbia adui, kuteketeza silaha za vita, kukiuka amri na kushiriki katika vitendo vya wizi.
Baada ya kusilizwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili, wanajeshi 25 wakiwemo makapteni wawili wamehukumiwa kifo. Wakili Muvweko amesema kuwa wanatazamia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Wakili huyo anayewatetea wanajeshi hao wa Kongo ameongeza kuwa, watuhumiwa wengine wakiwemo wanawake wanne wameachiwa huru kwa kukosekana ushahidi.
Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita kundi la waasi wa M23 limeteka miji kadhaa kaskazini mwa mstari wa mbele wa mapambano. Kusonga mbele kwa waasi wa M23 ni pamoja na kuudhibiti mji wa kimkakati wa Kanyabayonga ambao unahesabiwa kama lango kuu kuelekea katika vituo muhimu vya biashara vya Butembo na Beni.
Miaka kadhaa iliyopita waasi wa M23 waliyateka maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; ambapo walikaribia kuudhibiti kikamilifu mji wa Goma, makao makuu ya mkoa wa Kivu Kusini huku wakiuwa makumi ya watu na kulazimiisha mamia ya maelfu ya wengine kuhama makazi yao.
Serikali ya Kinshasa inaituhumu Rwanda kuwa inawaunga mkono waasi wa M23; tuhuma ambazo zimekanushwa na Kigali.
Mapema mwezi Mei mwaka huu wanajeshi wanane wa Kongo, wakiwemo maafisa watano walihukumiwa kifo huko Goma kwa "uoga" na "kuwakimbia adui".