Jul 20, 2016 16:11 UTC
  • Mapigano ya kikabila yauwa na kujeruhi watu kadhaa Kivu Kaskazini

Watu kadhaa wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano ya kikabila yaliyojiri katika kijiji kimoja mkoani Kivu ya Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Duru za kijeshi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimetangaza kuwa, watu kumi wameuawa na sita kujeruhiwa kwenye mapigano kati ya makabila ya Wahutu na Nande katika kijiji cha Kibirizi mkoani Kivu Kaskazini.

Kwa miaka mingi maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hayajawahi kushuhudia utilivu na amani hata siku moja.

Baadhi ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

 

Duru hizo zimeongeza kuwa  wanajeshi wa Kongo wameshindwa kuzuia kuuliwa watu kwenye mapigano hayo licha  ya kutumwa kusimamisha mapigano. Duru za kijeshi za Kongo zimesisitiza kuwa wakazi wa kijiji cha Kibirizi wana wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea mapigano mapya ya kikabila kijijini hapo. Habari zinasema kuwa wakazi wa Kibirizi hivi sasa wanayakimbia makazi yao kufuatia kushadidi machafuko katika kijiji hicho. Maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa. Kushindwa jeshi la Kongo na wanajeshi wa kofia bluu kuwaangamiza wanamgambo katika maeneo hayo, kumepelekea kuongezeka na kuenea ukosefu wa amani mashariki mwa nchi hiyo.

Tags