Kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu yaanza nchini Sudan
(last modified Sun, 20 Oct 2024 10:32:32 GMT )
Oct 20, 2024 10:32 UTC
  • Kampeni ya chanjo dhidi ya kipindupindu yaanza nchini Sudan

Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa, imeanzisha kampeni ya chanjo kwa ajili ya kuwafikia zaidi ya watu milioni 1.4 ikiwa ni sehemu ya kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu katika maeneo ya mashariki na kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya wizara hiyo imesema: "Awamu ya hivi sasa ya kukabiliana na mripuko unaoendelea hivi sasa wa kipindupindu ilizinduliwa jana (Jumamosi) asubuhi katika majimbo matatu ya Mto Nile (kaskazini mwa Sudan), Kassala na Gedaref (mashariki mwa Sudan)." 

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: "Kampeni hii inakusudia kutoa chanjo kwa watu 1,407,546 wenye umri wa mwaka mmoja na kuendelea na itaendelea hadi siku ya Alkhamisi."

Wakati huo huo, Ismail Al-Adani, Mkurugenzi wa Mpango wa Chanjo katika Wizara ya Afya ya Sudan amesema kuwa, dozi zaidi za chanjo ya kipindupindu zitawasili nchini humo tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba.

 

Wizara hiyo imeongeza kuwa, tarehe 5 Oktoba ilipokea dozi milioni 1.4 za chanjo ya kipindupindu iliyotolewa na shirika la kimataifa la GAVI, Shirika la Afya Duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF).

Sudan imeharibiwa vibaya na vita vya uchu wa madarakani baina ya manejerali wa kiijeshi wanaoongoza makundi mawili ya SAF na RSF tangu tarehe 15 Aprili 2023. 

Wizara ya Afya ya Sudan imesema kuwa, hadi hivi sasa imesajili kesi 25,037 za kipindupindu na vifo 702 vinavyohusiana na ugonjwa huo.

Juzi Ijumaa, UNICEF ilionya kwamba watu milioni 3.1 wakiwemo watoto 500,000 walio na umri wa chini ya miaka 5, wako katika hatari ya ugonjwa wa kipindupindu nchini Sudan.