Jul 23, 2016 16:50 UTC
  • Jeshi la Nigeria laapa kukomboa maeneo yanayoshikiliwa na B/Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa litaendeleza mashambulizi yake hadi kukombolewa maeneo yote yanayodhibitiwa na kundi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kamanda wa ngazi ya juu wa kikosi maalumu cha Nigeria kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, Lucky Ilabor ameashiria tukio la kutoweka wanajeshi 19 na wapiganaji wa kujitolea katika shambulio la kuvizia la magaidi wa Boko Haram dhidi ya maeneo ya jeshi huko Maiduguri na kusisitiza kuwa, kundi la Boko Haram litalipa gharama kubwa kwa kitendo hicho.

Ilabor amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vinafanya juhudi za kuwatambua na kuwaangamiza wanamgambo wengi wenye mfungamano na Boko Haram.

Kushindwa kwa kiasi fulani serikali na jeshi la Nigeria kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram kumesababisha raia wengi kuuawa katika mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi.

Nigeria na nchi nyingine jirani yaani Chad, Niger, Cameroon na Benin mwaka jana zilikubaliana kuunda jeshi lenye wanajeshi, polisi na maafisa wa kiraia 8700 kwa mijalili ya kuendesha mapambano makubwa dhidi ya Boko Haram kwa uungaji mkono na Umoja wa Afrika (AU).

Watoto wanaotumiwa katika vita Nigeria

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) Jumanne iliyopita ulitangaza kuwa watoto wadogo wanatumiwa katika mashambulizi ya kujilipua ya Boko Haram na kwamba mashambulizi mengi zaidi hutekelezwa katika maeneo ya raia nchini Nigeria. Unicef imesema kiwango hicho  cha utumiaji watoto kimeongezeka mara kumi ikilinganishwa na mwaka 2015.

Tags