Jul 25, 2016 04:19 UTC
  • Operesheni dhidi ya Boko Haram yakabiliwa na uhaba wa mafuta

Kamanda Mkuu wa vikosi vya ulinzi vya Nigeria amesema kuwa, uhaba wa mafuta ya ndege za kijeshi kwa sasa ndilo tatizo kuu linaloikabili operesheni ya kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Jenerali Abayomi Gabriel Olonisakin amesema kuwa, uhaba wa mafuta ya ndege za kijeshi umekuwa na taathira hasi kwa operesheni dhidi ya Boko Haram. Kwa mujibu wa jeshi la Nigeria operesheni hiyo inaendeshwa katika eneo la Ziwa Chad kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Jeshi la Nigeria likiwasaka wapiganaji wa Boko Haram

Hayo yanajiri katika hali ambayo, jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, litaendeleza operesheni zake hadi kuyakomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram nchini humo.

Baadhi ya mabinti waliookolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram

Licha ya hivi karibuni jeshi la Nigeria kuonekana kupata mafanikio katika operesheni yake dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram na hata kufanikiwa kuwaokoa mamia ya wanawake na watoto waliokuwa wakishikiliwa mateka na wanamgambo hao, lakini serikali ya Rais Muhammadu Buhari ingali inaandamwa na ukosoaji kutokana na kushindwa kulitokomeza kundi hilo la wanamgambo.

Wanachama wa Boko Haram wanaosifika kwa mauaji

Hivi karibuni Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa kundi hilo la Boko Haram

 

Tags