Afrika Kusini kugeukia Russia, Iran kwenye mradi wake wa nyuklia?
(last modified Tue, 18 Feb 2025 07:32:56 GMT )
Feb 18, 2025 07:32 UTC
  • Afrika Kusini kugeukia Russia, Iran kwenye mradi wake wa nyuklia?

Afrika Kusini imesema huenda itashirikiana na Russia au Iran katika juhudi za kupanua uwezo wake wa nishati ya nyuklia.

Shirika la habari la Mehr limeripotii habari hiyo na kuongeza kuwa, Afrika Kusini, ambayo inaendesha kinu pekee cha nishati ya nyuklia barani Afrika cha Koeberg, inapanga kuongeza megawati 2,500 za nishati, ili kukabiliana na uhaba wa umeme ambao umeathiri uchumi. Lengo jingine la kuimarisha mradi wake wa kiraia wa nyuklia ni kupunguza uchafuzi wa hewa unaotokana na gesi chafu.

Waziri wa Madini na Rasilimali za Petroli wa Afrika Kusini, Gwede Mantashe amesema, "Hatuwezi kuwa na mkataba unaotuzia kuipa Iran au Russia zabuni, hatuwezi kuwa na hali hiyo."

Kwa mujibu wa Reuters, Mantashe ambaye ni mmoja wa watetezi wakuu wa serikali wa kutaka kupanuliwa uwezo wa nyuklia wa nchi hiyo amesisitiza kuwa, "Tutakhitari (nchi) yoyote ikiwa ndilo chaguo bora zaidi kwenye meza."  

Pretoria kwa sasa haina ushirikiano wa pande mbili na Iran juu ya nishati ya nyuklia au teknolojia yoyote inayohusiana na nyuklia, Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa imesema.

Baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza kuikatia misaada Afrika Kusini kutokana na eti sera zake za unyakuzi wa ardhi, Mantashe alisema kuwa, mataifa ya Afrika hayapaswi kuogopa vitisho vya Marekani. "Tuzuie madini kwenda Marekani, sisi sio ombaomba, tuitumie jaala hiyo (madini) kwa manufaa yetu. Kama bara iwapo tutadumaa kwa hofu, tutaanguka."