Algeria yawafukuza majajusi 2 wa Ufaransa kwa kuingia nchini na pasi za bandia za kusafiria
Serikali ya Algeria imewafukuza maajenti wawili wa ujasusi wa Ufaransa kwa kuingia nchini humo kwa kutumia "pasi bandia za kidiplomasia " ikiwa ni ishara mpya ya kuongezeka mvutano kati ya nchi mbili hizo.
Televisheni ya kimataifa ya Algeria imetangaza kuwa majasusi hao wawili walikuwa wakifanya kazi katika Kurugenzi ya Usalama wa Ndani katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, na hawafuta taratibu za kisheria wakati wa kuingia Algeria.
Televisheni ya Algeria imetaja tukio hilo kuwa ni ujanja ulioratibiwa na Bruno Retailleau Wazri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa. Hadi tunaandika taarifa hii, hakukuwa na maelezo yoyote kutoka kwa upande wa Ufaransa kuhusiana na majasusi wake hao.
Algeria imewafukuza majasusi hao wawili wa Ufaransa ikiwa imepita wiki chache tangu Algeria iwafukuze wafanyakazi 12 wa ubalozi wa Ufaransa mapema mwezi Aprili mwaka huu katika kulipiza kisasi kutiwa nguvuni mfanyakazi wa ubalozi wake mdogo mjini Paris kwa madai ya kuhusika katika kumteka nyara mwanaharakati wa upinzani wa nchini Algeria.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Algeria na Ufaransa bado ni tete, hasa kutokana na kadhia zilizosababishwa na ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria kuanzia mwaka 1830 hadi 1962 ambazo hazijapatiwa ufumbuzi hadi sasa