Kufukuzwa wanadiplomasia; Je, kwa mara nyingine Algeria imeasi dhidi ya Ufaransa?
Huku mvutano ukishadidi katika uhusiano wa kisiasa kati ya Ufaransa na Algeria, nchi hizo mbili zimewafukuza wanadiplomasia kadhaa kutoka katika nchi zao.
Uhusiano wa Algeria na Ufaransa kwa mara nyingine tena umegubikwa na mzozo na mvutano katika siku chache zilizopita. Mvutano huo ulianza baada ya kukamatwa mfanyakazi wa ubalozi mdogo wa Algeria huko Ufaransa. Maafisa wa Ufaransa wanadai kuwa, mtu huyo, pamoja na raia wengine wawili wa Algeria, walihusika katika utekaji nyara wa Amir Boukhors, mwanaharakati wa kisiasa na mkosoaji wa serikali ya Algeria, ambaye alitekwa nyara katika viunga vya Paris mnamo Aprili 2024.
Kukamatwa kwa watu hao kumeibua mgogoro mpya katika uhusiano kati ya Algeria na Ufaransa, ambapo Algeria imewafukuza wanadiplomasia 12 wa Ufaransa katika hatua ambayo haijawahi kushuhudiwa. Kwa hakika, mamlaka za Algeria zimetangaza kukamatwa kwa mfanyakazi wa ubalozi wa nchi hiyo kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mikataba ya kidiplomasia. Kitendo hiki cha Algeria, kilisababisha Ufaransa kulipiza kisasi kwa kuwafukuza wanadiplomasia 12 wa Algeria na kumrudisha nyumbani balozi wake kutoka Algiers.
Uhusiano wa Ufaransa na Algeria umekuwa wa mvutano, hasusan katika miaka ya hivi karibuni. Mvutano huu umezidi kuwa mbaya katika miezi ya hivi karibuni baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kuunga mkono misimamo ya Morocco katika mzozo wa Sahara Magharibi. Hivi majuzi Ufaransa ilitangaza katika barua kwa Mfalme wa Morocco, Mohammed VI kwamba, hali ya sasa na ya baadaye ya Sahara Magharibi iko ndani ya mfumo wa mamlaka ya Morocco na kwamba Ufaransa inaiunga mkono. Mabadiliko haya ya kimsimamo ya Ufaransa yaliikasirisha sana Algeria.
m

Maafisa wa Algeria waliuelezea msimamo wa Ufaransa kuwa unatokana na hesabu za kisiasa zenye kutia shaka na utoaji hukumu wa kimaadili wenye kutiliwa shaka na kufuatia hayo mivutano kati ya nchi hizo mbili iliongezeka. Kufuatia mzozo huu wa miezi kadhaa, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa Jean-Noël Barrot hivi karibuni alisafiri hadi Algeria katika juhudi za kuboresha uhusiano, na baadaye akatangaza kwamba uhusiano kati ya Algiers na Paris unarejea katika hali ya kawaida. Hii ni katika hali ambayo, filihali kwa mara nyingine tena mzozo mkubwa umeonekana tena wazi katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Weledi wa mambo wanaamini kwamba, mizizi ya mzozo wa sasa inapaswa kutafutwa katika uhusiano wa zamani kati ya Ufaransa na Algeria.
Ukoloni wa Ufaransa nchini Algeria na ukandamizaji ambao umewafanyia Waalgeria, kwa upande mmoja, na mkusanyiko wa tabia za kiburi na kutowajibika katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kukataa kuwajibika kwa uhalifu wa enzi ya ukoloni, kuhodhi vyombo vya habari dhidi ya Algeria, na majaribio ya kushawishi taasisi za ndani za nchi hiyo, kwa upande mwingine, kumesababisha raia wa Algeria kutokubali tena kufuata siasa na matakwa ya Ufaransa.
Ukweli wa mambo ni kuwa, hatua ya sasa ya Algeria ya kuwafukuza wanadiplomasia inaonyesha hasira zaidi ya Waalgeria kuliko hapo awali. Waalgeria hawako tayari tena kuvumilia mwelekeo mpya wa ukoloni wa Ufaransa katika nchi yao. Kuhusiana na hili, taasisi za usalama za Algeria zimesema kwa uwazi kwamba shughuli za kidiplomasia za Ufaransa nchini Algeria zimevuka mfumo wa maingiliano ya kawaida na zimepenya na kuingia katika maeneo ya "usalama wa taifa na masuala ya kiintelijensia."

Kwa muktadha huo, kufukuzwa kwa wanadiplomasia 12 wa Kifaransa sio hatua ya kihisia na kimhemko, bali ni uamuzi ulioratibiwa wa kupunguza nyanja za ushawishi wa siri wa Paris katika masuala ya ndani ya Algeria. Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa hatua hii, mamlaka ya Algeria kwa mara nyingine tena imetangaza kwa Ufaransa kwamba, zama za diplomasia ya udhalilishaji zimepita na kwamba lazima iheshimu uhuru na mamlaka ya kitaifa ya Algeria, heshima ya kihistoria, na uhuru wa kweli katika uhusiano wa kisiasa.
Kwa maneno mengine ni kuwa, kuwafukuza wanadiplomasia hao sio tu jibu la papo hapo kwa mzozo wa kisiasa; bali ni radiamali yenye mizizi dhidi ya kuendelea ya mawazo ya kikoloni katika sera za Ufaransa kwa koloni lake la zamani.
Katika uwanja huo, kama Ufaransa inataka kudumisha uhusiano wa kawaida na Algeria, basi lazima kwanza ikubali ukoloni wake uliopita na kufikiria upya sera zake. Inaonekana kwamba Algeria haitaki tena idhini ya nchi za Magharibi, hasa Ufaransa; badala yake, inatafuta ushirikiano sawa kwa misingi ya kuheshimiana.