WFP yadondosha misaada Sudan Kusini kutokea angani kutokana na mapigano
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, (WFP) limeanza kudondosha misaada ya dharura ya chakula kwa njia ya anga kwa maelfu ya familia katika Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini, ambako mapigano yaliyopamba moto tangu mwezi Machi mwaka huu yamewafanya watu walazimike kuhama makazi yao na kukaribia kuzitumbukiza baadhi ya jamii kwenye njaa ya kupindukia.
Taarifa iliyotolewa na WFP katika mji mkuu Juba imesema, mgao huo ni wa kwanza kutolewa na shirika hilo katika kipindi cha zaidi ya miezi minne, na unalenga kuokoa maisha kwa zaidi ya watu 40,000 wanaokabiliwa na njaa kali katika maeneo ya mbali ya kaunti za Nasir na Ulang, ambayo yanaweza kufikishiwa misaada kwa kudondoshewa kutokea angani tu.
Mary-Ellen McGroarty, Mkurugenzi wa WFP nchini Sudan Kusini amesema “kwa masikitiko makubwa uhusiano kati ya mzozo na njaa ni dhahiri Sudan Kusini, na tumeshuhudia hili katika miezi iliyopita huko Upper Nile. Bila kuongeza msaada huu kwa kiwango kikubwa, kaunti za Nasir na Ulang ziko katika hatari ya kuingia kwenye baa kamili la njaa. Tunahitaji kufikishia familia hizi chakula kwa haraka, na tunafanya kila juhudi kuwafikia wale wenye uhitaji zaidi kabla hali haijazidi kuwa mbaya.”
WFP inasema zaidi ya watu milioni moja jimboni Upper Nile wanakabiliwa na njaa kali, wakiwemo zaidi ya watu 32,000 wanaopitia viwango vya juu kabisa vya njaa au (IPC5) ambacho ni kiwango cha juu zaidi cha uhaba wa chakula.
Idadi hiyo imeongezeka mara tatu tangu kuzuka kwa mapigano mwezi Machi, ambayo yamesababisha watu wengi kukimbia makazi yao, wakiwemo waliovuka mpaka kuelekea Ethiopia ambako WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu takribani 50,000 waliokimbia kutoka Upper Nile wakitafuta chakula na usalama.../