Matokeo ya awali, mchuano mkali katika uchaguzi wa rais Zambia
Mchuano mkali umeshuhudiwa katika uchaguzi wa rais nchini Zambia, huku Rais Edgar Lungu wa nchi hiyo na mshindani wake wa karibu Hakainde Hichilema wakipishana kwa mwanya mwembamba.
Tume ya Uchaguzi Zambia ECZ imesema yumkini matokeo hayo yasitangazwe leo jioni au kesho asubuhi kama ilivyoratibiwa, kutokana na kijitokeza idadi kubwa ya wapiga kura kinyume na matarajio.
Esau Chulu, mwenyekiti wa tume hiyo amesema kuwa, Rais Lungu amepata kura 17,620 katika maeneo bunge matatu, huku mpinzani wake mfanyabiashara mashuhuri Hichilema akipata kura 16,358.
Kwa mujibu wa sheria za Zambia, uchaguzi huo utaingia duru ya pili iwapo hakuna mgombea yeyote wa kiti cha urais atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura.
Wagombea 9 wamejitokeza kuwania kiti cha urais katika uchaguzi huo ambao ni wa tano kufanyika nchini humo katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.
Aidha katika uchaguzi huo wa Alkhamisi, wananchi waliwachagua wabunge, madiwani, mameya wa miji sambamba na kushiriki kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba.