85% ya matokeo ya kura Zambia, Rais Lungu aongoza
Rais Edgar Lungu wa Zambia angali anaongoza kwa kura chache dhidi ya mpinzani wake wa karibu, baada ya asilimia 85 ya kura za uchaguzi wa rais kuhesabiwa.
Tume ya Uchaguzi nchini humo ECZ imetangaza kuwa, katika matokeo ya maeneobunge 132 kati ya 156, Rais Lungu anaongoza kwa asilimia 50.1 huku hasimu wake wa karibu Hakainde Hichilema wa chama cha UPND akiwa na asilimia 47.7.
Hata hivyo kinara huyo wa upinzani na mfanyabiashara tajiri wa nchi hiyo ameeleza kutoridhishwa kwake na mwenendo na mwendo wa kinyonga wa kuhesabiwa kura hizo. Aidha amedai kuwa maafisa wa tume ya uchaguzi wanafanya uchakachuaji wa matokeo kwa maslahi ya Rais Lungu na kusisitiza kuwa lazima kura zihesabiwe upya katika wilaya ya kistratajia ya Lusaka.
Jana Jumapili, taarifa iliyotolewa na chama cha UPND ilieleza kuwa mfumo wao wa kuhesabu kura ulioenda sambamba na ule wa ECZ umeonyesha kuwa Hichilema amemshinda kwa kura za kutosha Lungu baada ya asilimia 80 ya kura zote kuhesabiwa. Maafisa wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia wamevionya vyama vya siasa kutoa taarifa za aina hiyo, hata hivyo vyama vyote vina uwezo wa kukusanya matokeo ya upigaji kura na kujumuisha matokeo kwa haraka zaidi kuliko tume hiyo.
Kinara wa upinzani na mshindani wa karibu wa Rais Lungu alipoulizwa na waandishi wa habari iwapo anaridhishwa na mwenendo wa kuhesabiwa kura na zoezi zima la uchaguzi amejibu "Jibu langu ni hapana! Siwezi kusema kuwa uchaguzi huu ni huru na wa haki."