Mashambulizi ya anga ya Marekani kaskazini mwa Libya yamegonga mwamba
Mchambuzi mmoja wa masuala ya Libya ameeleza kuwa mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani katika mji wa Sirte kaskazini mwa Libya kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh hayajazaa matunda.
Jason Pack mchambuzi wa masuala ya Libya na ambaye pia ni mwasisi wa Taasisi ya Eye on Isis ameashiria mashambulizi ya anga ya Marekani katika mji wa Sirte na kubainisha kuwa mashambulizi hayo hayatakuwa na natija nzuri kwa muda mrefu na kwamba mgogoro wa kisiasa nchini humo utasalia bila kupatiwa ufumbuzi.
Jason Pack ameongeza kuwa hata kama mji wa Sirte utakombolewa, lakini kundi la Daesh litaendelea kufanya mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya Libya. Mchambuzi huyo wa masuala ya Libya amesema kuwa nchi hiyo hivi sasa inahitaji mchakato mpana wa kisiasa na kwamba mashambulizi ya anga pekee hayatoshi.
Mji wa pwani wa Sirte huko kaskazini mwa Libya ulivamiwa na kudhibitiwa na magaidi wa kitakfiri wa Daesh tangu msimu wa joto mwaka jana. Hii ni katika hali ambayo nchi za Magharibi zimezidisha harakati na oparesheni zao za kijeshi huko Libya kwa kisingizio cha kupambana na kundi la Daesh; ambapo makamanda wa Marekani wapo huko Libya tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Agosti wakishirikiana na vikosi vya Uingereza katika mji wa Sirte. Bunge la Libya lenye makao yake mashariki mwa nchi pia limemuita balozi wa Marekani nchini humo na kumtaka atoe maelezo kufuatia mashambulizi ya anga yanayofanywa na ndege za Marekani huko Sirte.