Zoezi la kuhesabu kura nchini Uganda linaendelea
Shughuli za kuhesabu kura zimeanza katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kote Kampala na sehemu zingine za Uganda, baada ya kumalizika kwa zoezi la upigaji kura.
Mamlaka za Uganda zimewasihi wananchi kuendelea kuwa na subira na kuruhusu mchakato wa zoezi hilo la kidemokrasia uendelee kwa uwazi na bila kuingiliwa.
Zoezi la kupiga kura hii leo lilikumbwa na ucheleweshaji mkubwa wa suhula za kupigia kura, hitilafu za kiufundi, na hata vurumai katika baadhi ya vituo vya kupigia kura
Ikiwa kila kitu kitaenda kulingana na mpango wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, matokeo ya kura za urais yanapaswa kujulikana kufikia saa kumi alasiri kwa saa za nchi hiyo siku ya Jumamosi, Januari 17.
Raia zaidi ya milioni 21 wa Uganda wamepiga kura leo katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa kuendeleza utawala wa muda mrefu wa Rais Yoweri Museveni. Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa saa kumi alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.
Museveni mwenye umri wa miaka 81 na aliye madarakani tangu mwaka 1986, anawania muhula wa saba, huku kukiwa na hofu kuhusu uwazi wa mchakato huo hasa wakati huu kukiwa kumezimwa mtandao wa intaneti na mawasiliano.
Hata hivyo, Museveni anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mwanamuziki aliyegeuka mwanasiasa Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43, anayewakilisha kizazi kinachotamani mabadiliko ya kisiasa katika taifa la Afrika Mashariki lenye watu takribani milioni 45.
"Tunafahamu vyema kwamba wanapanga kuiba uchaguzi, kuwakandamiza watu vibaya, kuwaua watu, na hawataki ulimwengu wote uone," Bobi Wine ameliambia shirika la habari la AFP akizungumzia hatua ya serikali kuzimwa intaneti na kubanwa mawasiliano.