Miili ya watu 115 yapatikana kufuatia kuzama boti ya wahamiaji Misri
Waokoaji nchini Misri wamefanikiwa kupata miili zaidi katika Bahari ya Mediterranean baada ya boti iliyokuwa na mamia ya wahamiaji kuzama hivi karibuni karibu na pwani ya nchi hiyo.
Maafisa wa Misri wamesema wamepata miili 115 katika maji ya nchi hiyo baada ya boti iliyokuwa na wahamiaji kuzama siku ya Jumatano. Jitihada za kutafuta wale walionusurika na miili zaidi zinaendeshwa na jeshi la nchi hiyo na hadi sasa watu 163 wameokolewa. Boti hiyo ilikuwa na wahamiaji kutoka Misri, Syria, Sudan, Eritriea na Ethiopia.
Walionusurika wanasema boti hiyo ya uvuvi ilikuwa imepakia watu kupita kiasi kwani ilikuwa na wakimbizi 450 waliokuwa wakielekea Italia kabla ya kuzama kilomita 12 kutoka ufukwe wa bahari. Maafisa wa Misri tayari wameshawakamata washukiwa wane wanaosafirisha binadamu kinyume cha sharia.
Takwimu mpya za Shirika la Wahajiri Duniani zinaonyeshah kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 hadi sasa, wahajiri karibu laki moja na elfu tano; ambao wengi walitokea Libya walifanikiwa kuingia nchini Italia. Katika kipndi hicho wanaume, wanawake na watoto 2,726 pia walizama majini kabla ya kufika katika nchi waliyokuwa wakielekea.
Aidha kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, tangu mwaka 2014 hadi sasa zaidi ya wahajiri elfu 10 waliokuwa wanaelekea Ulaya kupitia njia ya bahari, wamepoteza maisha.
Wahamiaji hao haramu wengi wao wamekuwa wakitokea katika nchi za Libya, Misri, Algeria, Morocco, Somalia, Sudan na Ethiopia.