Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali ya boti Misri yapindukia 200
Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali ya kupinduka kwa meli iliyobeba wahamiaji haramu iliyotokea wiki iliyopita kwenye eneo la Bahari ya Mediterranean imefikia 202.
Habari kutoka tovuti ya gazeti la Piramidi ya Misri zinasema abiria wengi zaidi ni Wamisri, na wengine ni wahamiaji haramu kutoka nchi nyingine za Afrika.
Tarehe 21 mwezi huu wa Septemba, boti iliyobeba wahamiaji haramu 600 hivi ilipinduka kwenye eneo la Bahari ya Mediterranean. Hadi sasa watu 163 wameokolewa, na wengine wengi hawajulikani walipo.
Walionusurika wanasema boti hiyo ya uvuvi ilikuwa imepakia watu kupita kiasi wakimbizi waliokuwa wakielekea Italia kabla ya kuzama kilomita 12 kutoka ufukwe wa bahari. Maafisa wa Misri tayari wameshawakamata washukiwa wanne wanaosafirisha binadamu kinyume cha sheria.
Takwimu mpya za Shirika la Wahajiri Duniani zinaonyesha kuwa tangu kuanza mwaka huu wa 2016 hadi sasa, wahajiri karibu laki moja na elfu tano; ambao wengi walitokea Libya walifanikiwa kuingia nchini Italia. Katika kipindi hicho wanaume, wanawake na watoto 2,726 pia walizama majini kabla ya kufika katika nchi waliyokuwa wakielekea.
Aidha kwa mujibu wa Kamishna Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, tangu mwaka 2014 hadi sasa zaidi ya wahajiri elfu 10 waliokuwa wanaelekea Ulaya kupitia njia ya bahari, wamepoteza maisha.
Wahamiaji hao haramu wengi wao wamekuwa wakitokea katika nchi za Libya, Misri, Algeria, Morocco, Somalia, Sudan na Ethiopia.