Ripoti: Majeshi ya Sudan yametumia silaha za kemikali dhidi ya raia Darfur
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16306-ripoti_majeshi_ya_sudan_yametumia_silaha_za_kemikali_dhidi_ya_raia_darfur
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limevituhumu vikosi vya serikali ya Sudan kwamba, vimetumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 29, 2016 04:10 UTC
  • Ripoti: Majeshi ya Sudan yametumia silaha za kemikali dhidi ya raia Darfur

Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limevituhumu vikosi vya serikali ya Sudan kwamba, vimetumia silaha za kemikali dhidi ya raia katika jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo.

Ripoti ya Amnesty International iliyotolewa leo imeeleza kuwa, vikosi vya serikali ya Sudan vilitumia silaha za kemikali dhidi ya raia baina ya mwezi Januari hadi Septemba mwaka huu katika mashambulio yake dhidi ya waasi huko Darfur.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa, katika mashambulio hayo kwa uchache raia 30 waliuawa huko Jabal Murrah katika jimbo la Darfur. Ripoti ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International inatolewa huku duru mpya ya mazungumzo ya kitaifa ya Sudan ikitarajiwa kuanza tarehe 10 ya mwezi ujao wa Oktoba katika mji mkuu Khartoum.

Wakimbizi wa Darfur

Kwa muda mrefu jimbo la Darfur lililoko magharibi mwa Sudan limekuwa likishuhudia machafuko na ukosefu wa usalama na kuyafanya maisha ya wakazi wa jimbo hilo kuwa hatarini.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa, watu zaidi ya laki tatu wameuawa katika machafuko ya Darfur yaliyoanza mwaka 2003 na wengine milioni mbili na nusu wamelazimika kuwa wakimbizi.

Aidha mashirika mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakitahadharisha mara kwa mara kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika jimbo hilo na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za kuzuia kutokea maafa ya kibinadamu.