Rais Rouhani: Hali ya Yemen ni ya kusikitisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17179-rais_rouhani_hali_ya_yemen_ni_ya_kusikitisha
Rais Hassan Rouhani amesema hali ya Yemen ni ya kusikitisha na amekosoa mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2016 04:33 UTC
  • Rais Rouhani: Hali ya Yemen ni ya kusikitisha

Rais Hassan Rouhani amesema hali ya Yemen ni ya kusikitisha na amekosoa mashambulio ya kinyama yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo jana mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kurejea nchini kutoka safari yake ya kutembelea nchi kadhaa za kusini mashariki mwa bara la Asia.

Rais Rouhani amesema: "Hali ya Yemen ni ya kusikitisha kwa sababu wananchi madhulumu wasio na hatia ambao hawana hali nzuri ya kiuchumi, kwa muda wa miaka miwili sasa wametingwa na mashambulio ya makombora ya serikali ya Saudia". 

Dakta Rouhani ameongezea kwa kusema:" Kwa kweli huwezi kuamini kwamba katika mwezi ulioharamishwa vita na umwagaji damu wa Muharram, wao wanaendelea bila ya sababu yoyote kuwaua watu ambao ni ndugu zao Waislamu wakiwemo wanawake na watoto".

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyaeleza hayo kufuatia shambulio la kinyama lililofanywa hivi karibuni na Saudi Arabia nchini Yemen.

Mashambulio ya Saudia Yemen yamesababisha maafa makubwa

Katika moja ya mashambulizi yake ya kinyama zaidi kuwahi kufanya dhidi ya Yemen, siku ya Jumamosi ndege za kivita za muungano vamizi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud zilishambulia kwa makombora shughuli ya mazishi ya baba wa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Yemen mjini Sana'a ambapo watu zaidi ya 140 waliuawa na mamia ya wengine walijeruhiwa.

Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zimelaani shambulio hilo la anga; navyo vikosi vya jeshi la Yemen vimetangaza kuwa vitazidisha mashambulio yake na kuhakikisha vinatoa jibu dhidi ya jinai hiyo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu zaidi ya 10,000 wameshauawa hadi sasa tangu Saudia ilipoanzisha uvamizi na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Yemen mwezi Machi mwaka uliopita.../