Waislamu 10 wauawa Nigeria katika kumbukumbu ya Ashura
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17278-waislamu_10_wauawa_nigeria_katika_kumbukumbu_ya_ashura
Watu wasiopungua 10 wameuawa leo katika mapigano yaliyotokea baina ya jeshi la Nigeria na Waislamu waliokuwa katika maombolezo na kumbukumbu ya mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali katika jimbo la Katsina huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Oct 12, 2016 12:29 UTC
  • Waislamu 10 wauawa Nigeria katika kumbukumbu ya Ashura

Watu wasiopungua 10 wameuawa leo katika mapigano yaliyotokea baina ya jeshi la Nigeria na Waislamu waliokuwa katika maombolezo na kumbukumbu ya mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali katika jimbo la Katsina huko kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Ripoti zinasema kuwa, jeshi la Nigeria limeshambulia mkusanyiko wa Waislamu waloikuowa katika maombolezo na Ashura na shughuli ya kukumbuka tukio chungu la kuuliwa shahidi Imam Hussein (as) katika mji wa Funtua na kuua watu wasiopungua 10 wakiwemo wanawake. Makumi ya Waislamu wengine wakiwemo watoto wadogo wanashikiliwa na polisi ya Nigeria. 

Jeshi la Nigeria limetumia gesi ya kutoa machozi kutawanya waombolezaji na kuwatia mbaroni baadhi yao. 

Ghasia na mauaji hayo ya Katsina yametokea baada ya jeshi la Nigeria kuzingira msikiti wa Waislamu waliokuwa katika maombolezo ya siku ya tisa ya mwezi Muharram, Tasua, katika jimbo la Kaduna na kuwatia nguvuni Waislamu wasiopungua 15. 

Wanawake na watoto wadogo waliokamatwa leo Funtua

Ghasia na mashambulizi kama hayo ya jeshi la Nigeria pia yameshuhudiwa pia katika maeneo na majimbo mengine ya nchi hiyo dhidi ya Waislamu hususan wa madhehebu ya Shia ambao katika siku hizi wanakumbuka tukio chungu la kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein bin Ali (as). 

Disemba mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia Waislamu wa mji wa Zaria jimboni Kaduna na kuua mamia miongoni mwao. Jumuiuya za kutetea haki za binadamu zinasema jeshi la Nigeria liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo. 

Waislamu waliouawa na jeshi la Nigeria, Kaduna 2015

Imam Hussen aliuawa shahidi mwaka 61 Hijria akiwa pamoja na jamaa na wafuasi wake 72 walisimama kupambana na mtawala dhalimu wa kizazi cha Bani Umayyah, Yazid bin Muawiya, aliyebadili na kupotosha mafundisho ya Uislamu.