Rais wa CAR awataka wananchi wadumishe mshikamano wa kijamii
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amewatolea wito wananchi na makundi ya kijeshi nchini humo kufanya mapatano ya kitaifa.
Rais Faustine Archange Touadera wa Jamhuri ya Afrika ya Kati amesema kuwa, anawaomba wananchi wadumishe mshikamano na umoja wa kitaifa. Rais Touadera ameitaja suluhu ya kitaifa kuwa ndiyo njia pekee inayoweza kuisadia Jamhuri ya Afrika ya Kati kuondokana na hali ya mchafukoge na vita vya ndani vinavyoisumbua hivi sasa. Ameongeza kuwa duru mpya ya machafuko na mapigano ya ndani imepelekea kubomolewa nyumba za raia, kuwafanya maelfu ya watu kuwa wakimbizi na kuirudisha nchi katika hali ya huko nyuma kwa gharama na hasara kubwa.
Jamhuri ya Afrika ya Kati imekuwa ikitatizwa na mapigano makali ya kikaumu na kikabila na hivyo kuitumbukiza nchi hiyo katika hali ya mchafukoge tangu katikati ya mwaka 2013.
Rais Faustine Archange Touadera ambaye alishika hatamu za kuiongoza nchi hiyo miezi sita iliyopita, amesema kuwa moja ya masuala anayoyapa umuhimu katika uongozi wake ni kuiona Jamhuri ya afrika ya Kati inakuwa na amani na makundi ya wanamgambo yanapokonywa silaha. Hata hivyo nchi hiyo hadi sasa ingali inakabiliwa na mivutano na hitilafu za ndani.