Asasi za kiraia CAR: Wakimbizi wanakabiliwa na hali mbaya ya kibinaadamu
Asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya kibinaadamu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, zimeonya juu ya hali ambaya ya kibinaadamu inayowakabili wakimbizi wa taifa hilo.
Ripoti iliyotolewa na asasi hizo imeelezea hali mbaya waliyonayo maelfu ya wakimbizi wa eneo la Kaga-Bandoro, kaskazini mwa nchi hiyo, kutokana na kukosa nyenzo na zana muhimu za kiafya na chakula.
Kadhalika asasi hizo zimetoa indhari ya kibinaadamu kufuatia mapigano yanayoendelea baina ya wanachama wa kundi la Anti-Balaka na Seleka tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Oktoba, ambayo yamesababisha makumi ya raia kuuawa na mamia ya wengine kuwa wakimbizi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo Shirika la Madaktari wasio na mipaka hivi karibuni limetangaza kuwa kwa kuzingatia kushadidi machafuko hayo, limelazimika kufunga ofisi zake nchini humo. Wakati huo huo taarifa iliyotolewa na asasi zisizo za kiserikali nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, zimeelezea kukithiri vitendo vya uharibifu na uporaji wa mali za ofisi za Shirika hilo la Madaktari wasio na mipaka ambavyo vinafanywa na wanamgambo wenye silaha.